• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakulima wazindua kiwanda cha kahawa cha Sh4m

Wakulima wazindua kiwanda cha kahawa cha Sh4m

ALEX NJERU na STEPHEN MUNYIRI

WAKULIMA wa kahawa katika Kaunti ya Tharaka-Nithi sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya kuzindua kiwanda cha kusaga kahawa kilichogharimu Sh45 milioni.

Hii ni baada ya vyama 30 vya ushirika kutoka kaunti hiyo kuungana kisha kukopa Sh40 milioni ambazo walitumia kujenga kiwanda hicho huku serikali ya kaunti nayo ikiwananunulia mashine ya kusaga kahawa kwa kima cha Sh5 milioni.

Akizungumza wakati wa kuzinduliwa kwa kiwanda hicho, Gavana wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki alisema kwamba lengo lake ni kufufua kilimo cha kahawa ambacho kilikuwa kimeshamiri eneo hilo miaka ya 80.

Bw Njuki alisema analenga kushirikiana na vyama vya ushirika vya wakulima ili kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa.

“Lengo langu kuu ni kuvumisha kilimo cha kahawa kwa kuwaokoa wakulima ambao jasho la limekuwa likiliwa na wafanyabiashara laghai,” akasema Bw Njuki.

Kiongozi huyo alisikitika kwamba baadhi ya wakulima waling’oa majani ya kahawa kwenye mashamba yao na kupanda mimea mingine ili kupata fedha baada ya sekta ya kahawa kukumbwa na changamoto kadhaa na kuwasababishia hasara kubwa.

Mwenyekiti wa vyama vya ushirika vya wakulima Julius Riungu naye aliwashauri wakulima wote kuwasilisha mazao yao ya kahawa katika kiwanda hicho badala ya kuyapeleka katika viwanda vingine.

Kwingineko chama cha ushirika cha kahawa cha Baricho katika Kaunti ya Nyeri kinaelekea kuporomoka baada ya wakulima wenye hasira kukataa kupitisha makadirio ya kila mwaka ya bajeti wakilalamikia ubadhirifu wa fedha zao.

Wiki jana, wanachama wa kamati simamizi ya chama hicho chenye wanachama 500 kinachopatikana katika Kaunti ndogo ya Mathira Mashariki waliondolewa ofisini wakati wa mkutano wa kila mwaka ulioandaliwa katika kiwanda cha Karindundu.

Wakati wa mkutano huo, wakulima walikataa kupitisha bajeti ya kugharimia shughuli za kiwanda, wakisema ajenda kuu ilikuwa kuwaondoa wanachama wa kamati simamizi, hali ambayo sasa inatishia kusitisha shughuli zote za kiwanda hicho.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Baricho Wachira Wamwago alitaja tukio hilo kama siasa za kawaida zinazoshuhudiwa katika sekta ya kilimo cha kahawa.

You can share this post!

Mirengo ya ‘Embrace’ na ‘Inua Mama’ yakosolewa

Adhani kapata mke kumbe kicheche

adminleo