Uhuru aendelea kutua katika ngome kuu za Raila

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa katika Kaunti ya Mombasa Jumatatu, siku mbili baada ya kuzuru Kisumu ambako alikagua miradi ya maendeleo.

Ziara ya Rais mjini Kisumu ilikuwa ya kwanza kufanyika bila kuandamana na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, tangu aingie mamlakani 2013.

Leo akiwa Mombasa, ambayo pia ni ngome ya kisiasa ya Bw Odinga, Rais Kenyatta anatarajiwa kuzindua rasmi Chuo cha Mafunzo ya Mambo ya Majini (Bandari Maritime Academy) katika Bandari ya Kilindini.

“Kupitia chuo hicho, serikali inalenga kushughulikia upungufu wa wataalamu wa majini nchini Kenya na katika kanda hii ili kutimiza mahitaji ya sekta ya uchumi wa majini,” ikasema taarifa ya msemaji wa Ikulu Bi Kanze Dena.

Rais Kenyatta amekuwa akipata mapokezi mazuri katika ziara zake mjini Mombasa kutoka kwa Gavana Hassan Joho tangu aliporidhiana kisiasa na Bw Odinga mwaka jana.

Bw Joho, ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, alikuwa kiongozi wa kwanza kukumbatia muafaka huo na kutangaza kuzika tofauti zake za kisiasa na Rais Kenyatta.

Bw Odinga alikagua shughuli za ukarabati katika bandari ya Kisumu mnamo Alhamisi, lakini sasa yuko nchini Niger kwa mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).

Rais Kenyatta alirejea Kisumu wiki tatu baada ya kuzuru bandari hiyo akiandamana na Bw Odinga.

Kiongozi wa taifa alikuwa ametoka Tanzania ambako alikuwa amemtembelea Rais wa nchi hiyo John Magufuli nyumbani kwake eneo la Geita katika kile kilichotajwa kama ziara ya kibinafsi.

Rais Kenyatta alikuwa hajamtembelea rasmi Dkt Magufuli tangu aanze kuongoza Tanzania miaka minne iliyopita, isipokuwa kukutana kwenye mikutano.

Rais Kenyatta aliapa kuanza ziara zake pembe tofauti za Kenya ili kuzima kampeni za kikundi cha ‘Tangatanga’ wakati alipokemea vikali kikundi hicho wiki chache zilizopita.

Kwenye mahojiano ya awali, Msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena alisema ziara za Rais zitamfikisha maeneo tofauti ya nchi ikiwemo eneo la Kati ambako viongozi na wananchi hudai ametelekeza.

Tangu wakati huo, Rais amezuru pia Rift Valley alipozindua upya kiwanda cha nguo cha Rivatex mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Habari zinazohusiana na hii

Huu ni mzaha tu!

Hacheki na Uhuru

Funzo kwa Uhuru