Bwire shujaa akiongoza Sharks kurarua Everton mbele ya mashabiki 64,000
Na GEOFFREY ANENE
Wenyeji Kariobangi Sharks walijikakamua mbele ya mashabiki wao na kulemea mabingwa mara tano wa Kombe la FA Everton kutoka nchini Uingereza 4-3 kwa njia ya penalti katika makala ya tatu ya SportPesa Trophy katika uwanja wa Kasarani uliofurika mashabiki wapatao 64,829, Jumapili.
Muda wa kawaida ulitamatika 1-1 baada ya Duke Abuya kufungia Sharks katika kipindi cha kwanza naye Joe Williams akajaza bao la Everton mapema katika kipindi cha pili.
Katika upigaji wa penalti, kipa Brian Bwire alipangua penalti mbili na pia kufunga ya ushindi. Timu zote mbili zilianza vibaya kupiga penalti baada ya Willams na Abuya kupoteza. Nathan Broadhead, Josh Bowler, Fraser Hornby walifunga penalti zao tatu zilizofuata, huku Sharks ikifunga penalti tatu kabla ya Bwire kupangua penalti ya Dennis Adeniran na kisha kufuma ya ushindi.
Kipindi cha kwanza kilitamatika mabingwa wa SportPesa Shield mwaka 2018 Sharks wakiongoza 1-0 kupitia bao safi kutoka kwa mshambuliaji Abuya aliyemwaga kipa Mholanzi Maarten Stekelenburg kupitia shuti la katikati ya miguu yake.
Sekunde chache baadaye, Bwire aliondosha hatari kutoka kwa raia wa Senegal Ouma Niasse. Geoffrey Lemu karibu asawazishie Everton akiondosha hatari dakika chache baadaye. Hata hivyo, korna aliyosababisha haikuzalisha bao.
Harrison Mwendwa kisha alipata nafasi nzuri ya kuongezea Sharks bao la pili alipopokea pasi nzuri pembeni kulia dakika ya 33, lakini alivuta shuti ambalo halikupata mchezaji wa Sharks na likapita mbele ya goli.
Nafasi nzuri kabisa ya Everton katika dakika 45 za kwanza ilipatikana dakika ya 39 pale Theo Walcott alipiga krosi nzuri ndani ya kisanduku, lakini kizibo cha Ademola Lookman, Broadhead alipiga nje shuti akiwa mbele ya lango.
Beki Mason Holgate na kiungo Mreno Andre Gomes walilishwa kadi ya njano kila mmoja katika kipindi cha kwanza kwa kuchezea Eric Kapaito na Sven Yidah, mtawalia.
Everton ilirejea kipindi cha pili na bidii na kusawazisha kupitia ikabu ya Williams iliyosababishwa na Thomas Teka. Williams alipiga shuti la chini. Vijana wa Marco Silva walinyuka Gor Mahia 2-1 mwaka 2017 na 4-0 mwaka 2018.
Rekodi ya mashabiki ya mechi za Kenya:
Agosti 26, 1989 – Misri na Kenya (Nasser, Misri) mashabiki 100,000
Agosti 12, 1987 – Kenya na Misri (Kasarani, Nairobi) 80, 000
Januari 24, 1999 – DR Congo na Kenya (Kinshasa) 75, 000
Februari 27, 1977 – Misri na Kenya (Nasser) 70, 000
Januari 12, 1997 – Kenya na Nigeria (Kasarani, Nairobi) 65, 000
Julai 7, 2019 – Kariobangi Sharks (Kenya) na Everton (Uingereza) 64,829
Agosti 1, 1987 – Kenya na Tunisia (Kasarani, Nairobi) 60, 000
Mei 13, 2018 – Gor Mahia (Kenya) na Hull City (Uingereza) 60, 000
Agosti 17, 2005 – Tunisia na Kenya (Tunis) 60, 000
Aprili 27, 1997 – Kenya na Guinea (Nairobi) 57, 000
Aprili 20, 1985 – Nigeria na Kenya (Lagos) 50, 000
Juni 18, 2005 – Kenya na Morocco (Nyayo, Nairobi) 50, 000