Uhuru akwepa Mlima Kenya
Na MWANGI MUIRURI
HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru maeneo mengi ya nchi akizindua miradi ya maendeleo huku akikwepa eneo la Mlima Kenya imezua manung’uniko miongoni mwa wakazi na viongozi wa Kati.
Hii ni baada yake kukosa kuonekana eneo hilo akizindua ama kukagua miradi ya maendeleo kama anavyofanya katika ngome za upinzani.
Mara ya mwisho Rais kuonekana Mlima Kenya kwa shughuli za maendeleo ilikuwa Novemba 2018 alipofungua soko jipya la Karatina, Kaunti ya Nyeri.
Aprili mwaka huu Rais alikuwa amepangiwa kufanya ziara eneo la Mlima Kenya akiandamana na kinara wa upinzani, Raila Odinga lakini zikaahirishwa na hadi sasa hatima yake haijulikani.
Rais Kenyatta husisitiza analenga kupeleka maendeleo katika kila pembe ya nchi bila kujali kama ni eneo lililompigia kura au la.
Lakini wadadisi wanaona uamuzi wa serikali yake kutilia maanani ustawi maeneo fulani hasa Nyanza kuwa unatokana na mtindo mpya wa siasa zinazochezwa na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.
Wikendi Rais Kenyatta alizuru Kisumu kukagua ukarabati wa bandari ya Kisumu ambayo amepangiwa kufungua upya mwezi ujao. Jana alikuwa Mombasa kufungua taasisi ya mafunzo ya ubaharia.
Manung’uniko ya wakazi wa Mlima Kenya yamekuwa yakionyeshwa kupitia kwa wanamuziki wa eneo hilo, ambao wamechomoa wakimsuta kiongozi wa nchi kwa kile wanachosema ni kuwasahau waliomuunga mkono kuingia Ikulu.
Wengine wanahisi kuwa kila mara anapozuru eneo hilo akiwa kwenye hafla zingine kama za kidini ama mazishi amekuwa akitumia fursa hizo kuwazomea viongozi wa eneo hilo wanaoonekana kukosoa serikali yake.
“Hawa washenzi wananiambia kuwa nimebakisha risasi moja ya kisiasa…watashangaa! Wanasema kuwa wanataka wakutane nami. Mimi nimewapa mawaziri wa kuongea nao lakini wakishindwa na kazi wananisingizia,” akasema Rais wakati wa uzinduzi wa soko la Karatina.
Mwezi uliopita akiwa kwenye mkutano wa Akorino uwanjani Kasarani, Rais aliwakemea vikali viongozi wa Mlima Kenya hasa wanaojitambulisha na kundi la ‘Tangatanga’ linalomuunga mkono Naibu Rais William Ruto.
Lakini Ikulu imepuzilia mbali madai kuwa Rais Kenyatta anahepa ngome yake ya kisiasa.
“Mawaziri wote wa kushirikisha ajenda nne kuu za serikali ni wa Mlima Kenya. Kuna Sicily Kariuki (Afya), James Macharia (Uchukuzi), Peter Munya (Viwanda na Biashara) na Mwangi Kiunjuri (Kilimo). Sasa unashindwa wanamtaka Rais awatuze kingine kipi,” akasema afisa wa ngazi ya juu Ikulu.
“Rais anafaa ajiulize kama kwa kweli anatendea Mlima Kenya haki anapoonekana akizindua miradi ya maendeleo kwingine na ngome yake kumejaa manung’uniko,” asema aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo.
Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri anasema kuwa Rais amewatenga wakazi wa eneo la Kati huku akiwadhalalisha viongozi ambao wanamkosoa.
“Tukimwambia tukutane ili tujadiliane, anahepa. Tukisema tuko tayari kumtafuta tujadiliane kuhusu masuala nyeti ya eneo hili, anatutusi,” akasema Bw Ngunjiri.
Seneta wa Nyeri, Ephraim Maina anasema Rais yuko kwenye njia panda kutokana na haja kuwa sharti aonekane kuwa na msimamo wa kitaifa.
“Tunajua kuwa Rais ni wa kitaifa. Lakini hafai kuogopa ukweli kwamba Mlima Kenya ni sehemu ya taifa hili. Akiwajibikia maeneo mengine ya taifa, hata nasi tunahitaji huduma sawa na hizo anazotoa katika maeneo mengine,” akasema Bw Maina.
Kwa mujibu wa wakili Ndegwa Njiru, ambaye pia ni mchanganuzi wa kisiasa katika eneo hilo, hii sio mara ya kwanza kwa rais kuchaguliwa kisha anakosa kushughulikia maslahi ya wenyeji.
“Watu wa Mlima Kenya wamegeuzwa kuwa wacheza ngoma ya kutwaa mamlaka, lakini wakati wa kutuza, wao hugeuzwa kuwa mashabiki wa kushangilia kikombe kikikabidhiwa wengine waliokuwa nje ya mchezo huo,” asema Bw Njiru.
Anaeleza kuwa licha ya eneo la Kati kutoa marais watatu, Mzee Jomo Kenyatta, Mzee Mwai Kibaki na Rais Uhuru Kenyatta, hakuna cha kujivunia kimaendeleo katika eneo hilo.