Punda aundiwa miwani baada ya kuumia jicho
MASHIRIKA Na PETER MBURU
PUNDA ambaye alipofuka baada ya kujeruhiwa vibaya katika ajali nchini Uingereza amenunuliwa miwani spesheli, ili kumsaidia kuona tena.
Punda huyo alijeruhiwa baada ya kukanyaga mwiba, lakini athari za majeraha zikaathiri hadi macho, kiwango cha kupoteza uwezo wa kuona.
Hata hivyo, mnyama huyo amepata afueni baada ya kutengenezewa miwani spesheli, ambayo itazuia macho yake yasiathirike na miale hatari ya jua.
Hii ni baada ya kutibiwa na madaktari spesheli wa mifugo katika hospitali ya Sidmouth, Devon.
“Punda huyo aliathirika vibaya machoni baada ya kudungwa mguuni, tukishuku alikuwa na mawazo mengi. Alikuwa na vidonda vya tumbo, alikuwa akilia na alionekana kuwa na uchungu mwingi,” daktari wa kuchinja mifugo Vicky Grove akasema.
Wafanyakazi katika hospitali hiyo walimpa miwani ili awe akiona vyema, bila kuathirika.
“Tangu tumpe miwani, amekuwa akiendelea vyema,” akasema daktari huyo.
Punda huyo anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya mifugo eneo hilo.