• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
Kampuni za maji Murang’a zahimizwa zisambaze maji kote bila ubaguzi

Kampuni za maji Murang’a zahimizwa zisambaze maji kote bila ubaguzi

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI tano za maji katika Kaunti ya Murang’a zimehimizwa kufanya haki kuona ya kwamba zinasambaza maji kwa kila sehemu inayostahili kupata bila ubaguzi wa aina yoyote.

Afisa mkuu wa kitengo cha maji katika Kaunti ya Murang’a, Bw Anthony Maina maarufu Maina wa Mai, amesema inasikitisha kuona ya kwamba maji yanasambazwa kwa ubaguzi katika baadhi ya maeneo katika kaunti hiyo.

Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano kuhusu usambazaji wa maji kwa mwananchi wa kawaida.

“Mwananchi wa chini katika kijiji anastahili kupata maji kila wakati bila ubaguzi lakini kwa wiki za hivi karibuni kumekuwa na mvutano wa kila mara kwa kampuni hizo huku zikisambaza maji kwa kubagua sehemu fulani.,” amesema Bw Maina.

Amesema matarajio ya Gavana wa Murang’a, Bw Mwangi Wa Iria, ni kuona ya kwamba maji yanasambazwa katika kila boma kwa sababu hakuna upungufu wowote kwa sasa.

Amependekeza kuwa ni vyema kampuni hizo tano zije pamoja na kuwa kampuni moja kwa minajili ya kutumikia mwananchi kwa sauti moja.

Tatizo la maji

Ameyasema hayo mjini Murang’a ambapo alizuru kijiji cha Kiagage, eneo la Kiharu ambako wananchi wamekuwa na shida ya maji kwa wiki kadha mfululizo.

Amewahimiza viongozi Murang’a kuunga mkono ajenda muhimu za Kaunti hiyo ili mwananchi wa kwaida aweze kunufaika pakubwa na maendeleo.

Pia amemhimiza mbunge wa Kandara Bi Alice Wahome kushirikiana na Kaunti ya Murang’a ili wananchi wanufaike vilivyo.

Ameahidi kufanya juhudi kuona ya kwamba bomba la maji lililopasuka sehemu za Gaichanjiru limerekebishwa mara moja.

Amesema Kaunti ya Murang’a inataka kumaliza shida ya maji Murang’a yote ili kila mwananchi apate maji katika boma lake.

“Lengo langu kuu in kuona ya kwamba kwa ushirikiano na viongozi wengine kila mkazi anafurahia maji katika boma lake ifikiapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2019,” alisema Bw Maina.

You can share this post!

Mwingereza aliyejijengea boma Kakamega azikwa

Simbas na Lionesses walipua wapinzani wao Uganda na...

adminleo