• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mafuriko yasababisha vifo zaidi

Mafuriko yasababisha vifo zaidi

Na WAANDISHI WETU

TAKRIBAN watu 15 wamekufa na wengine kujeruhiwa huku mali yenye thamani ya mamilioni ya pesa ikiharibiwa na mvua kubwa ambayo imeendelea kunyesha sehemu tofauti nchini.

Ijumaa asubuhi, Wakenya walikuwa wakiomboleza na wengine kuhesabu hasara iliyosababishwa na mvua katika maeneo ya Nairobi, Mlima Kenya, sehemu za Pwani na Kaskazini Mashariki.

Baadhi ya wanafunzi wa kutwa pia walilazimika kulala shuleni baada ya njia wanazotumia kuelekea nyumbani kuathiriwa na mvua hiyo.

Katika kaunti ya Machakos, maiti nne zilitolewa kutoka Mto Athi, katika daraja la Joska-Kamulu kwenye barabara kuu ya Nairobi-Kangundo, Ijumaa asubuhi.

Mkuu wa polisi Matungulu, Bw Samuel Mukuusi alisema waathiriwa walikufa maji walipokuwa wakivuka mto uliofurika Alhamisi usiku.

Daraja hilo lilibebwa na maji mto ulipopasua kingo zake kufuatia mvua kubwa ya Alhamisi.

Katika kaunti ya Kitui, watu watano walifariki baada ya kubebwa na maji katika mto Enziu, kaunti ndogo ya Mwingi Mashariki, Alhamisi.

Vilevile Kaunti za Nakuru na Narok, mafuriko yalisababisha vifo vya watu watatu Jumatano usiku waathiriwa wakiwa ni pamoja na mwanafunzi wa sekondari.

Watoto wawili wenye umri wa miaka minane na miaka mitatu, pia walikufa maji katika matukio tofauti Alhamisi jioni walipojaribu kuvuka Mto Mwatate.

Polisi walieleza kuwa mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi ya Maili Kumi alikuwa akielekea nyumbani kutoka shule alipokumbana na kifo chake.

Na katika eneo la Mwatate, mvulana mwenye umri wa miaka mitano alibebwa na maji akijaribu kuvuka Mto Mwatate.

Mvulana mwenye umri wa miaka minane pia alikufa maji katika eneo la Taveta alipokuwa akiogelea katika chimbo lililowachwa wazi eneo la Lesesia.

Afisa Mkuu wa polisi, Bw Fred Ochieng alisema kuwa babake mtoto huyo alipiga ripoti kuwa mwanawe alikuwa akilisha mbuzi alipokufa maji. Katika Kaunti ya Meru, mwanamume alibebwa na mafuriko eneo la Mugae, barabara ya Ruiri-Isiolo Alhamisi jioni.

Mshirikishi wa Shirika la Msalaba Mwekundu eneo la Kati, Bw Gitonga Mugambi alisema kuwa mwanamume mwingine aliokolewa alipojaribu kuvuka barabara hiyo akiwa kwa pikipiki.

Watu wengi walikwama barabarani na wengine kulazimika kutumia njia zingine kutokana na mafuriko.

Bw Mugambi alieleza kuwa kuna haja ya wasimamizi kutekeleza marufuku ya shughuli zinazoendelea kwa migodi hadi mvua iwache kunyesha ili kuzuia vifo.

 

You can share this post!

Ulikuwa uamuzi mchungu sana kukutana na Uhuru – Raila...

Je, ni nembo ya ‘usaliti’ kwa Raila kumkumbatia Uhuru?

adminleo