Magavana kuandamana kupinga wabunge kujiongezea hela
NA SHABAN MAKOKHA ALEX NJERU na CHARLES WASONGA
MAGAVANA na maseneta wametishia kuandamana katika Bunge la Kitaifa Jumatatu kulalamikia mvutano unaozingira kiasi cha fedha zinazopasa kutengewa serikali za kaunti.
Magavana hao walisema wataandamana katika majengo ya bunge, Nairobi kutaka wabunge waeleze sababu ya kupinga nyongeza ya fedha kwa serikali za kaunti.
“Tutaungana na maseneta katika maandamano hayo Jumatatu kuonyesha kuwa ugatuzi unauawa na Bunge la Kitaifa,” akasema Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati.
Alikuwa miongoni mwa magavana saba waliokutana mjini Kakamega Ijumaa kuhudhuria sherehe ya uzinduzi wa mpango wa kuwapiga jeki kiuchumi vijana na wanawake katika kaunti hiyo.
Magavana hao walilalamikia mvutano kati ya maseneta na wabunge kuhusu suala hilo na ambao ulikwamisha kupitishwa kwa mswada huo kabla ya kusomwa kwa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020.
Wengine walioungana na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya katika sherehe hiyo ni Paul Chepkwony (Kericho), Prof Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Cornel Rasanga (Siaya), Ali Roba (Mandera) na Mwangi wa Iria (Murang’a).
Walidai Bunge la Kitaifa linatumiwa na Serikali Kuu kuhujumu utekelezaji wa ugatuzi.
“Kile tunachoshuhudia sasa ni sawa na kilichotendeka 1966 serikali kuu ilipoua utawala wa majimbo,” alisema Bw Wangamati ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Rasilmali katika Baraza la Magavana (CoG).
Bunge la Kitaifa na Hazina ya Kitaifa, zinapendekeza kuwa serikali za kaunti zigawiwe Sh310 bilioni katika mwaka huu wa kifedha huku Seneti na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) zikipendekeza mgao wa Sh335 bilioni.
Bw Oparanya ambaye ni Mwenyekiti wa CoG alisema huenda shughuli katika kaunti zikakwama na hata zikakosa pesa za kuwalipa wafanyakazi ikiwa mvutano huo hautatatuliwa.
Wakati huo huo, Naibu Rais William Ruto amewashauri magavana kushiriki mazungumzo kutatua mvutano kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) badala ya kwenda kortini huku magavana na maseneta wakipanga kufanya maandamano kesho kuhusu suala hilo.