• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WANDERI: Vijana tulizeni boli, ndoa ni safari ndefu!

WANDERI: Vijana tulizeni boli, ndoa ni safari ndefu!

Na WANDERI KAMAU

HAFLA ya kufana ya harusi kati ya Gavana wa Kirinyaga, Bi Ann Waiguru na wakili Kamotho Waiganjo inapaswa kutufunza kuwa hakuna umri ambao mtu hawezi kumpata mpenzi wake wa kweli.

Wawili hao walikuwa katika ndoa za awali, lakini wakaachana na wanandoa wao kupitia talaka.

Kando na kuwa katika umri mpevu, wawili hao pia wana watoto.

Harusi yao ya kipekee, ambayo ilifanyika jana katika Kaunti ya Kirinyaga, inajiri wakati visa vya wapenzi kuuawa nchini vimeongezeka sana.

Wale waliojipata katika utandu huo wa mauaji ni vijana, hasa walio katika miaka ya ishirini na thelathini.

Kando na Bi Waiguru, wengine walioonyesha mfano mzuri ni aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom, marehemu Bob Collymore na Bi Wambui Kamiru, ambao pia walikuwa katika ndoa za awali kabla ya kuoana.

Bw Collymore alikiri kwamba alikuwa ameoa mara tatu na kutalikiana mara mbili, kabla ya kumpata Bi Kamiru.

Pengine hii ni mifano tosha kwa vijana kuwa suala la mapenzi huwa halitaki pupa, ila ni hatua muhimu inayohitaji umakinifu mkubwa kwa kila mmoja.

Katika maisha ya mwanadamu hapa duniani, ndoa huorodheshwa kama hatua ya tatu katika hatua nne kuu, ambazo ni kuzaliwa, kupashwa tohara, ndoa na kifo.

Kwa tathmini ya kina, ndoa ndiyo hatua muhimu zaidi, kwani huwa mwamuzi mkuu wa maisha atakayoishi aliyeoa ama aliyeolewa.

Ndoa pia huwa haihitaji shinikizo zozote kutoka kwa jamii, kwani ni baadhi ya sababu hizo ambazo zimekuwa zikiwafanya wanandoa wengi kutalikiana ama kushambuliana wanapokosana.

Katika mafundisho mengi ya dini mbalimbali, wanandoa hushauriwa kuwa ni “wamoja” hivyo hawawezi kutengana wakati tofauti zinapoibuka kati yao.

Kwa mfano, katika dini ya Kikristo, wanandoa hawapaswi kupeana talaka, ikiwa sababu za tofauti zao hazitokani na mmoja wao kuwa mwasherati.

Hilo bila shaka linawafunga, hali ambayo inawalazimu kuvumiliana hata ikiwa wanakosana kwa misingi ya ‘kutii’ kanuni na mafundisho ya dini.

Kwa namna moja ‘utumwa’ huo ndio umekuwa kiini cha wanandoa wengi kuuana, kwani huchukulia ndoa kama ‘gereza’ waliloundiwa na imani zao za kidini.

Sheria kali za kidini zinazodhibiti ndoa huwafanya wanandoa kushindwa hata kusuluhisha matatizo madogo ambayo yangehitaji suluhisho rahisi.

Licha ya nchi za Magharibi kuorodheshwa kuwa miongoni mwa zile zinazoongoza kwa idadi kubwa ya talaka, angaa kuna mifano michache inayoonyesha umuhimu wa msamaha na kuvumiliana.

Mfano bora ni hatua ya Bi Hillary Clinton kumsamehe mumewe, Bill Clinton kufuatia sakata yake ya mapenzi na mwanadada Monicah Lewinsky mnamo 1998.

Hilo linaonyesha kuwa wawili hao hawakuwa chini ya shinikizo zozote kuingia katika ndoa.

Vivyo hivyo, lazima vijana wajifunze kuwa nyakati za kufikia hatua mbalimbali katika maisha ya mwanadamu huwa tofauti; kuna wanaotangulia na wanaofuata.

Bora tu, kila mtu atafika. Wanaweza kujijenga kabla ya ndoa. Haraka ni ya nini?

[email protected]

You can share this post!

Polo afumaniwa kwa jirani akiwa uchi

OBARA: Mbona serikali inawaruhusu mabroka wa mahindi...

adminleo