TAHARIRI: Knut ilegeze masharti yake makali dhidi ya TSC
NA MHARIRI
SEKTA ya elimu imekuwa ikikumbwa na misukosuko mingi kwa miezi kadhaa sasa.
Ukosefu wa utulivu katika sekta hii unasababishwa na mambo mengi ikiwemo utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu na mizozo baina ya vyama vya walimu na mwajiri wao kuhusu uhamisho na kupandisha walimu vyeo.
Hii leo, kuna mambo mawili makuu yanayotarajiwa kufanyika katika sekta hii.
Kwanza, Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kimetangaza kujitolea kwake kukutana na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ili kutatua mizozo iliyopo kati yao.
Ijapokuwa Knut imefanya vyema kwa kueleza imejitolea kushauriana na TSC, bado kuna tatizo kwani wawakilishi wa muungano huo wanatoa misimamo mikali hata kabla ya mkutano kufanyika.
Inaeleweka Knut inaposhikilia kwamba ni sharti maagizo yaliyotolewa na korti wiki iliyopita kuhusu malalamishi yao yatekelezwe, lakini haifai viongozi wa muungano huo kutishia mgomo endapo TSC itaamua kukata rufaa.
Ukataji rufaa kuhusu uamuzi wowote wa mahakama ni haki iliyolindwa kisheria, na ikiwa Knut inataka TSC isichukue mwelekeo huo, haifai kutumia vitisho bali viongozi wakubali kukutana kwanza na kuona jinsi utekelezaji utakavyofanywa, na ikiwa kuna changamoto, ni mwelekeo upi utachukuliwa kwa manufaa ya pande zote mbili.
Jambo la pili kuu ambalo linatarajiwa leo ni uzinduzi wa vikao vya kukusanya maoni ya wananchi na wadau kuhusu utekelezaji kikamilifu wa mtaala mpya.
Mtaala huo ambao ulianza kutekelezwa katika madarasa ya chini ya msingi, uliibua mgawanyiko mkubwa miongoni mwa walimu wanaopinga, na serikali ambayo imesisitiza kuendelea na hatua zake ilivyopangwa.
Ni matarajio yetu kwamba serikali itakuwa tayari kutekeleza maoni ya wengi yatakayotolewa kuanzia leo, hata ingawa hili ni jambo ambalo lingefanywa kabla utekelezaji kuanza.
Wakati misukosuko inapokumba sekta ya elimu, waathiriwa wakuu huwa ni watoto hasa wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani ya kitaifa.
Mwelekeo mwafaka wa kutatua changamoto zozote zilizopo katika sekta hii ni kupitia kwa mashauriano ya wadau wote.