• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
Hofu Gilgil wakazi kushuku wanalishwa nyama ya pundamilia

Hofu Gilgil wakazi kushuku wanalishwa nyama ya pundamilia

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa eneo la Gilgil na Naivasha, Nakuru wanahofia huenda wamekuwa wakila kitoweo cha pundamilia kwa muda sasa bila kujua.

Hii ni kutokana na ongezeko la visa vya mizoga inayopatikana imetupwa katika vichaka vya Gilgil na Weigh Bridge kilomita chache kutoka mjini Naivasha.

Ingawa baadhi yao wamekuwa wakilaumu magari ya uchukuzi wa umma kwa kusababisha ajali za kila mara, hili halifuti uwezekano kuwa nyama ya pundamilia inaliwa katika nyumba nyingi.

Baadhi yao waliokubali kuzungumza nasi wanasema ,huenda wahusika wamekuwa wakilindwa na polisi, kwani sio mara ya kwanza kisa kama hiki kutajwa.

Aidha John Kariuki (sio jina halisi) mfanyibiashara katika eneo la Gilgil anasema idadi ya pundamilia imepungua kiasi cha kushtua kinyume na siku za awali.

“Miaka michache iliyopita pundamilia walikuwa wengi na wakati mwingine kutatiza usafiri katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi lakini siku hizi wamepungua,”John akasema.

John aliongezea kuwa wahusika wamekuwa wakipata fursa rahisi, kuendeleza biashara hii kwa sababu eneo la Gilgil linashikana na makazi ya pundamilia.

Eneo la Gilgil ambapo wakazi wanahisi kuwa wanalishwa nyama ya pundamilia kutokana na idadi ya wanayama hawa kupungua kwa kasi baada ya muda mfupi. Picha/Richard Maosi

Wala hakuna uzio unaozingira sehemu yenyewe ili kutenganisha makazi ya watu na pundamilia.

“Isipokuwa Kagio Conservancy ambapo wanyama mwitu wametengewa sehemu yao maalum ya kuishi mbali na makazi ya watu ,na hawawezi kutangamana moja kwa moja na raia,”aliongezea.

Kulingana na John sio wauzaji wote wanaotekeleza biashara hii haramu isipokuwa ni wachache wanaotaka kuwaharibia wengine jina.

Eneo la Gilgil na Kikopey ni maarufu kwa uuzaji wa nyama choma za kila aina na biashara yenyewe inaendelea kutiliwa shaka.

Hili linajiri siku chache baada ya mshukiwa Samuel Gitome kufikishwa katika mahakama ya Nakuru mnamo Novemba 2018 kwa kupatikana na kilo 208 za nyama ya pundamilia.

Akisimama mbele ya hakimu mkuu mkazi wa Nakuru Josephat Kalo alipatikana na hatia ya kumiliki nyama ya pundamilia kinyume na sheria.

Mshtakiwa alipatikana na nyama ya pundamilia ikiaminika kutoka Soysambu ranch, lakini alikana mashataka hayo akidai ni maadui walimsingizia.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, mkugenzi wa afya ya umma Bw Samwel King’ori alisema mwezi wa Aprili aliwatahadharisha wakazi wa Nakuru dhidi ya kula nyama ambayo haijakaguliwa.

Aidha alieleza kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia njia ya mkato kujipatia pesa za haraka.

Maeneo yaliyolengwa zaidi yakiwa ni bucha,maduka ya kijumla na mikahawa inayoagiza idadi kubwa ya nyama.

You can share this post!

Mwanamke kortini kwa mazoea ya kushiriki ngono na maiti

Askofu kutumia helikopta kutimua mapepo jijini

adminleo