Griezmann kung'aa Barcelona kwa nambari 17 mgongoni
NA CECIL ODONGO
FOWADI wa Ufaransa Antoine Griezmann atavaa jezi nambari 17 baada ya kujiunga na vigogo wa soka ya Uhispania Barcelona kwa mkataba wa miaka mitano iliyogharimu Sh14 bilioni.
Kando na pesa hizo, Barcelona ililipa Sh92 bilioni iliyohitajika kabla ya mkataba wa mwanadimba huyo na Atletico Madrid kuvunjwa na kupisha uhamisho wake hadi uga wa Camp Nou.
Nambari hiyo ya kipekee iliwahi kuvaliwa na wachezaji waliovuma kambini mwa mabingwa hao wa La Liga kama Pedro, Mark van Bommel na Emmanuel Petit. Jeison Murillo ambaye alipelekwa kusakata kabumbu kwa mkopo kwenye klabu ya Valencia msimu uliopita wa 2018/19 ni mchezaji wa hivi punde kuvaa jezi yenye nambari hiyo inayothaminiwa sana Barcelona.
Akiwa amevalia jezi hilo Ijumaa Julai 12, Griezmann alieleza kwamba nia yake kuu ni kutwaa taji la Klabu Bingwa Barani Ulaya msimu wa 2019/20 ambao utang’oa nanga Agosti, 2019.
“Nimefurahi sana kuwa hapa. Kwa kweli natarajia kukumbana na mengi kwenye kabumbu nikiwa hapa na nipo tayari kupambana kiume
“Ni mwamko mpya. Huwa najaribu mara nyingi kutokaa kitako na kutazama mkondo wa mambo. Nataka kushinda mataji ya La Liga, Copa del Rey na lile la Klabu Bingwa Barani Ulaya ambalo sijalishinda kwenye taaluma yangu hadi sasa,” akasema Griezmann akiwa amejawa na tabasamu tele.
Baada ya kujiunga na Atletico kutoka Real Sociedad mwaka wa 2014, Griezmann aliwafungia mabao 133 katika mechi 257 alizosakata. Alishinda Ligi ya Uropa na Atletico Madrid katika msimu wa 2017-18.