• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Matiang’i awatimua wakurugenzi wa Sportpesa na Betin

Matiang’i awatimua wakurugenzi wa Sportpesa na Betin

Na PETER MBURU

SERIKALI Jumanne iliagiza wakurugenzi 17 wa kampuni za kamari ambao si raia wa Kenya watimuliwe mara moja.

Hii ni baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kuidhinisha kutimuliwa kwao, baada ya kutia sahihi nakala za amri za kutaka waondolewe nchini.

Kampuni hizo zinahusisha Sportpesa na Betin, ambazo hushiriki biashara ya kamari kwa watu kubashiri matokeo ya michezo, na ambazo zilipokonywa leseni na serikali baada ya kudaiwa zimekuwa zikikwepa kulipa ushuru.

Ripoti kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani ilisema kuwa sababu za amri za kutimuliwa kwa wakurugenzi hao nchini kwa kuwa wanashukiwa kushiriki katika biashara ya uchezaji Kamari, kinyume na walivyosema wanakuja kufanya walipoingia nchini.

Wengi wao ni wa kutoka mataifa ya mashariki mwa bara Uropa.

“Wengi wao walikiuka maagizo kuhusu kazi wanayofaa kufanya wakiwa nchini,” akasema msemaji wa wizara hiyo, Bi Wangui Muchiri.

Amri ya kutimuliwa kwa 17 hao imefika kama hatua ya punde zaidi kutoka kwa serikali dhidi ya kampuni za kamari baada ya kupiga marufuku akaunti za watu kutuma pesa ili kucheza michezo hiyo wiki iliyopita, kando na kupokonya kampuni 27 leseni za kuhudumu na pia kutaka benki kuzima akaunti zao

Kampuni zingine zilizopokonywa leseni ni Betway, Betpawa, Elitebet, PremierBet, Lucky2u, 1xBet, MozzartBet, Dafabet, World Sports Betting, Atari Gaming, Palms Bet na Betboss.

Zingine ni Kick-Off, Atari, Millionaire Sports Bet, Palmsbet, Chezacash, Betyetu, Bungabet, Cysabet, Saharabet, Easibet, Easleighbet, Sportybet na AGB Lottery & Gaming.

Dkt Matiang’i amekuwa akiapa kuadhibu kampuni hizo, akisema zinawafanya vijana wasio na kazi kutumia pesa katika uchezaji kamari badala ya kufanya kazi.

Jumatatu, maajenti wa kampuni hizo waliilaumu serikali kwa kushikilia msimamo mkali wa kusimamisha shughuli zao, wakiomba kikao na Dkt Matiang’i.

Kampuni ya Sportpesa pia Jumatatu iliweka tangazo katika gazeti kueleza jinsi iliendesha shughuli zake mwaka uliopita, kinyume na madai ya serikali kuwa ni mojawapo ya zile zilizokwepa kulipa ushuru, ikijitetea kuwa ililipa ushuru wa zaidi ya Sh9 bilioni, kati ya Sh20 bilioni ambazo ilipokea.

You can share this post!

Siwezi kutetewa na wakili wa kike, mshukiwa aambia korti

Jaribio la Kiunjuri kuagiza mahindi ugenini lazimwa

adminleo