• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 9:55 AM
Ada ya juu ya uegeshaji Nairobi yapendekezwa

Ada ya juu ya uegeshaji Nairobi yapendekezwa

NA MARY WANGARI

Waendeshaji magari jijini Nairobi watakabiliwa na nyakati ngumu siku za usoni ikiwa mswada uliopendekezwa na usimamizi wa Gavana Mike Sonko utapitishwa.

Hii ni baada ya afisa anayesimamia fedha katika baraza la kaunti Charles Kerich kuwasilisha mswada unaopendekeza waendeshaji magari kuanza kutozwa ada mbalimbali kutegemea eneo la uegeshaji.

Kulingana na ripoti ya gazeti la Daily Nation, watakaoegesha magari yao jijini watalipia kiasi cha Sh400 kila siku ambacho ni nyongeza ya asilimia 100 kutoka ada iliyokuwa ikitozwa awali ya Sh200.

Kwa upande mwingine, watakaotaka kuegesha magari yao viungani mwa jiji la Nairobi yakiwemo maeneo mengine ya kibiashara kama vile Westlands, Gigiri, Hurlingham miongoni mwa mengine watalazimika kutoa kiasi cha Sh300 kila siku.

Ada kwa watakaotaka huduma za uegeshaji katika maeneo mengine kando na haya itakuwa Sh 200 kwa siku.

Bw Kerich, katika kutetea pendekezo lake alihoji kwamba hatua hiyo ilikuwa muhimu muhimu katika kuongeza kiwangon cha mapato katika bajeti ya mwaka hui.

“Kaunti inafikiri kwamba mapendekezo hayo ndiyo yatakayoisaida kaunti kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kutoka kitengo cha uegeshaji,” alisema.

Aliongeza kwamba mapendekezo hayo yalikuwa katika Mswada wa Fedha 2019 uliowasilishwa mbele ya Tume ya Bajeti ya Baraza la Kaunti.

Haya yamejiri mwaka mmoja baada ya madiwani kufutilia mbali pendekezo sawa na hili ambapo ada ya uegeshaji ilipunguzwa hadi Sh200.

Japo mapato kutokana na ada ya uegeshaji magari yamekuwa kiini kikuu cha mapato ya Kaunti ya Nairobi huku kiasi cha Sh2 milioni kikikusanywa kila mwaka, limekuwa suala tata linalomfanya gavana pamoja na wadau husika kujikuna kichwa huku wakijaribu kudhibiti tatizo la msongamano wa trafiki jijini na wakati uo huo kuongeza kiwango cha ushuru unaokusanywa kutokana na ada ya uegeshaji magari jijini.

Katika siku za hivi majuzi, baraza la jiji limekabiliwa na kitendawili kigumu huku likijaribu kudhibiti mishahara ya wafanyakazi wake inayojumlisha asilimia 60 ya mapato yanayokusanywa na wakati uo huo kutengeneza barabara pamoja na kuondoa taka jijini.

You can share this post!

MAPITIO YA TUNGO: Asali Chungu; Riwaya inayoangazia athari...

Wavuvi walalamikia ukosefu wa vifaa vya kisasa

adminleo