Wavuvi walalamikia ukosefu wa vifaa vya kisasa
NA KALUME KAZUNGU
WAVUVI wa mpakani mwa Lamu na Somalia wanaitaka serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kuwafadhili kwa vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kutekeleza uvuvi kwenye bahari ya kina kirefu.
Ombi lao linajiri wiki chache baada ya serikali ya kitaifa kuondoa marufuku iliyowazuia wavuvi wa vijiji vya mpakani mwa Kenya na Somalia kutekeleza shughuli zao za uvuvi karibu na mpaka huo wan chi jirani kutokana na sababu za kiusalama.
Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Mshirikishi Mkuu wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata alizuru Lamu, hasa sehemu zote ambazo marufuku hiyo ilikuwepo na kutangaza kwamba serikali imeondoa marufuku hiyo hasa baada ya usalama kuimarishwa.
Mnamo Machi mwaka huu, Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i pia alizuru Lamu na kuamrisha wavuvi wote eneo hilo kusajiliwa kwa njia ya kielektroniki na kasha kuruhusiwa kuvua samaki baharin I usiku na mchana.
Katika mahojiano na wanahabari kwenye vijiji vya Kiunga, Ishakani, Ras Kamboni, Madina, Kiwayu, na Mkokoni, wavuvi walisema imekuwa vigumu kwao kupanua biashara hiyo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kutekelezea shughuli zao.
Wengi bado wanatumia mishipi, ndoano, nyavu na pia mashua na jahazi katika kutekeleza uvuvi wao, hatua ambayo wanadai imewazuia kutekeleza uvuvi kwenye bahari ya kina kirefu.
Bw Omar Mohamed ambaye ni mvuvi tajika mjini Kiunga alieleza haja ya kaunti na serikali ya kitaifa kuwafadhili wavuvi kwa boti za kisasa ambazo zina uwezo wa kupenya kwenye bahari ya maji mengi na kuwawezesha wavuvi kuendeleza shughuli zao kwenye maeneo hayo.
Pia aliitaka serikali kuwanunulia majokofu ya kuwawezesha kuhifadhi pato lao wakiwa baharini.
“Tunaishukuru serikali kwa kuturuhusu kutekeleza uvuvi usiku na mchana. Licha ya serikali kutuwachia uhuru huo wa kufanya shughuli zetu masaa yote, changamoto iliyopo na ambayo inazuia sekta ya samaki klupanuka ni ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kutekelezea shughuli hiyo. Wengi wetu bado unatumia mbinu za zamani katika kazi yetu. Tunaiomba kaunti na serikali ya kitaifa kutufadhgili kwa vifaa vya kisasa vya uvuvi,” akasema Bw Omar.
Bw Ahmed Islam ambaye ni mvuvi tajika eneo la Ishakani, alisema wavuvi wengi wamelazimika kusitisha shughuli zao kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kuendelezea biashara hiyo.
“Jahazi na mashua za zamani tunazotumia haziwezi kukimu dhoruba kali wakati ukijaribu kutekeleza uvuvi kwenye bahari ya kina kirefu. Tunalazimika kutekeleza uvuvi kwenye sehemu za bahari zinazokaribiana na ufuo. Sehemu hizi hazina samaki wengi ikilinganishwa na maeneo ya bahari ambayo ni ya kina kirefu. Baadhi yetu tumesitisha uvuvi kwa kushinda kukimu gharama ya vifaa vya kisasa vya kuboreshea uvuvi wetu. Tunahitaji msaada,” akasema Bw Islam.
Bi Amina Kombo alisema uvuvi ni tegemeo la kipekee kwa maisha ya wakazi hasa kwenye eneo la Lamu Mashariki.
Aliitaka serikali kuwasaidia wavuvi kuboresha uvuvi wao ili kuepuka umaskini ambao unazidi kukithiri miongoni mwa jamii.
“Takriban asilimia 90 ya wakazi wa eneo hili la Lamu Mashariki hutegemea uvuvi. Ikiwa wavuvi wanashindwa kwa kukosa vifaa, hiyo inamaanisha umaskini utazidi kutukumba. Serikali iingilie kati na kusaidia hawa wavuvi wetu kiuboresha shughuli zao. Wanunuliwe vifaa vya kisasa vya uvuvi,” akasema Bi Amina.