• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
ANN MWAI: Tajriba ya miaka 14 katika uigizaji

ANN MWAI: Tajriba ya miaka 14 katika uigizaji

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI ametunukiwa kipaji atakachotumia kufukuzia kutinga viwango vya kimataifa katika uigizaji. Ni takribani miaka 14 tangu aanze kujituma kwenye masuala ya uigizaji taaluma iliyomvutia tangu akiwa mdogo.

Aidha huyu ni binti anayejivunia kushiriki filamu nyingi tu na kupata mpenyo kurushwa kupitia runinga mbali mbali hapa nchini.

Ann Mwai analenga kumfikia kati ya waigizaji shupavu kimataifa aliye pia prodyuza mzawa wa Marekani, Julia Fiona Roberts. Anasema katika uhusika wake huvutiwa zaidi na filamu zake ikiwamo ‘My Best Friends Wedding’ na ‘Pretty Woman.’

Pia anatamani kufikia hadhi ya mwigizaji wa humu nchini Lupita Nyong’o anayeendelea kutesa katika filamu za Hollywood.

”Nina imani tosha kuwa endapo serikali itahakikisha vyombo vya habari nchini vinazingatia sheria ya kuonyesha asilimia 60 ya filamu za wazalendo sekta ya maigizo itapiga hatua na kutoa nafasi za ajira kwa waigizaji wanaokuja,” anasema.

”Nina furaha tele maana hivi karibuni nimeshiriki filamu fupi iitwayo ‘Rat a baby race’ ambayo imeteuliwa kuwania tuzo kwenye shindano la 7 Day Film Festival na kampuni ya filamu ya Seventy two media,” alisema na kuongeza kuwa ndiyo mwanzo wa ngoma lakini pia amepania kunasa tuzo katika uigizaji miaka ijayo.

Katika utangulizi wake mwaka 2004, alianza kushiriki michezo ya kuigiza kupitia mwongozo wa vitabu za riwaya ambapo alifanya kazi na makundi tofauti ikiwamo Planets Theatre production, Jicho 4, Starlight and Theatrix Arts Ensemble kati ya mengine.

Kuhusu kwa nini Wakenya hupenda kutazama filamu za kigeni anasema ”Dah! Nabii hakubaliwi kwao. Wakenya huvutiwa na filamu za kigeni maana ni nzuri kuliko kazi za wenzao wa hapa nchini.” Picha/ John Kimwere

Mwaka 2009 alipata fursa kufunza masuala ya maigizo chini ya mradi wa Amrefs Dagoretti Child in need, ambapo kipindi hicho pia akishirikiana na Chefu Macharia walipata fursa kuwa waandaji wa

kipindi cha Çhakula bora chini ya Theme Scape media walichokuwa wakirusha kupitia KBC Televisheni. Ameshiriki TV Series kama ‘The Dream’ na ‘Hope’or Mwihoko zilizorushwa kupitia Ebru TV na Inooro TV mtawalia.

Aidha anajivunia kushiriki filamu zaidi chini ya brandi tofauti kama: Urembo-Spilworks production, Twisted-Cheruscopic Production, The Dream-World of Mysteries, Hope-Jonvijo Production na Docudrama-Huriya kati ya zingine.

Kwa filamu ambazo huandaliwa na wanafunzi wanaosomea uanahabari katika chuo cha KIMC mwaka jana alishiriki filamu ‘Jipu’ ilhali mwaka huu ameshiriki filamu iitwayo ‘Siri ya Kaburi.’

Kando na filamu anajivunia kushiriki uigizaji wa sauti (voice over) kwa lugha tofauti ikiwamo Kiingereza, Kiswahili na Kikuyu ambazo hurushwa kupitia redio stesheni tofauti nchini.

Pia ameshiriki matangazo ya biashara ya bidhaa mbalimbali ikiwamo mkata wa Broadways, mabati ya Dumu Zas na Kaluma kati ya mengine.

Anadokeza kuwa hapa Kenya angependa kufanya kazi na waigizaji kama Lidya Gitachu ambaye ameshiriki filamu kama Kidnapped, Unseen, Unsung na Unforgotten. Pia Nice Githinji-All Girls together na Flowers nad Bricks.

Anasema sekta ya filamu imegubikwa na changamoto kibao maana nyakati zingine waigizaji hujikuta njiapanda hasa baada ya kufanya kazi na malipo yao kucheleweshwa.

You can share this post!

SADFA: Ezekiel Mutua asimulia kuugua kwa babake huku naye...

CAROLYNE KIARIE: Raha yangu ni kumfikia Gabriel Union...

adminleo