• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Wahadhiri watishia kumshtaki Magoha

Wahadhiri watishia kumshtaki Magoha

Na WANDERI KAMAU

Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Kenya (UASU) kimetishia kuenda mahakamani kupinga pendekezo la kuunganishwa kwa vyuo vikuu vya umma nchini, lililotolewa na Waziri wa Elimu Prof George Magoha.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Katibu Mkuu wa muungano huo Dkt Constantine Wasonga, alikosoa vikali pendekezo hilo, akisema linakiuka sheria zote zinazohusu kubuniwa ama kufutiliwa mbali kwa chuo kikuu chochote.

Prof Magoha alitoa pendekezo hilo mwanzoni mwa Juni, akisema lengo lake kuu ni kuboresha kozi zinazotolewa na vyuo vikuu vya umma.

Kabla ya kutoa tangazo hilo, waziri alisimamisha hatua ya vyuo vya umma kubuni mabewa zaidi, akisema a idadi ya vyuo vilivyopo inazidi ile inahitajika.

Lakini jana, UASU ililikosoa vikali, ikisema waziri hajazingatia taratibu za kubuniwa kwa vyuo, kulingana na Sheria ya Vyuo Vikuu ya 2012.

“Ni makosa kwa waziri kutoa pendekezo tu bila hata kuzingatia ikiwa linazingatia misingi ya kisheria. Tunapinga pendekezo hilo hadi pale taratibu zote za kisheria zitakapozingatiwa. Stakabadhi zetu ziko tayari. Tutafika mahakamani wakati wowote,” akasema Dkt Wasonga.

Kulingana na Prof Magoha, pendekezo hilo linatokana na hali kuwa vyuo vikuu vingi vya umma vimekuwa vikipata hasara, licha ya kuendelea kubuni mabewa mengi katika miji mbalimbali nchini.

Vyuo hivyo pia vimelaumiwa kwa kutozingatia ubora wa kozi vinavyotoa, kwani nyingi hazilingani na mahitaji ya sasa ya nchi.

Baadhi ya vyuo pia vimekosolewa kwa kubuni kozi hizo kwa haraka, lengo lake likiwa kupata idadi kubwa ya wanafunzi.

Kenya ina vyuo vikuu vya umma 31. Kulingana na rasimu ya mapendekezo hayo, idadi hiyo inakusudiwa kuwa kati ya vyuo 18 hadi 20.

Na licha ya UASU kutoa tishio hilo, ilisema kuwa waziri angengojea Bunge la Kitaifa kumaliza kujadili mapendekezo ambayo kimewasilisha kuhusu mpango huo.

“Hatupingi kuunganishwa kwa vyuo lakini mchakato unaofuatwa, kwani hatujashirikishwa hata kidogo kama wadau wakuu. Ni lazima waziri aache kuuendesha kibinafsi, bila kuwashirikisha wadau husika. Hii ni hatua muhimu, ambayo itakuwa na athari nyingi kwa maelfu ya wafanyakazi wanaohudumu katika taasisi hizo,” akasema.

Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Kutetea Wafanyakazi (TUC-Kenya) lilipinga mpango wa serikali kuanza kuwaajiri wafanyakazi wa mfumo wa kandarasi, likisema vile vile hauna msingi wa kisheria.

Kaimu Katibu Mkuu Dkt Charles Mukhaya alisema kuwa lazima washirikishwe kabla ya kutekelezwa kwake.

You can share this post!

Kina mama walevi watia wakazi hofu

TAHARIRI: Kaunti zizingatie ‘Punguza Mzigo’

adminleo