• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:10 PM
Ukosefu wa hela kwa Rwanda waipa Kenya tiketi ya bure U-20

Ukosefu wa hela kwa Rwanda waipa Kenya tiketi ya bure U-20

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya Kenya ya waunaume wasiozidi umri wa miaka 20 huenda ikapata tiketi ya bwerere kushiriki raundi ya pili mechi za kuingia Kombe la Afrika mwaka 2019.

Hii ni baada ya vyombo vya habari nchini Rwanda kuripoti kwamba wapinzani wa Kenya, Rwanda, hawana fedha za kutuma kikosi chao nchini Kenya kwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza baadaye mwezi huu.

Gazeti la New Times liliripoti Machi 17 kwamba Shirikisho la Soka nchini Rwanda (FERWAFA) liliwasilisha bajeti ya maandalizi ya timu ya Sh29, 938,213 katika Wizara ya Michezo, lakini likaambiwa na msemaji wa wizara hiyo Oleg Karambizib kwamba hakuna fedha.

Timu ya Kenya imekuwa ikijiandaa kualika Rwanda kati ya Machi 30 na Aprili 1 kabla ya kurudiana jijini Kigali kati ya Aprili 20 na Aprili 22. Kenya ilipangiwa kupimana nguvu na Tanzania na Misri mwezi huu wa Machi, lakini mechi hizo za kirafiki zikafutiliwa mbali.

Ukosefu wa fedha ukitupa Rwanda nje, basi Kenya itafuzu moja kwa moja kuchuana na mabingwa wa Afrika Zambia katika raundi ya pili itakayoandaliwa mwezi Mei mwaka 2018. Raundi ya tatu itaamua timu saba zitakazoshiriki Kombe la Afrika nchini Niger kutoka Februari 24 hadi Machi 10 mwaka 2019.

You can share this post!

‘Flash’ afikia rekodi ya Mehta kwenye Safari...

Mishahara ya maafisa wa polisi haifai kupunguzwa –...

adminleo