• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wavuvi Pwani walia fuo za bahari kunyakuliwa

Wavuvi Pwani walia fuo za bahari kunyakuliwa

Na SAMUEL BAYA

WAVUVI katika ukanda wa Pwani wamepoteza ekari nyingi za ardhi walizokuwa wakitumia katika ufuo wa bahari kwa wanyakuzi wa ardhi.

Ripoti iliyotayarishwa na taasisi moja ya utafiti katika eneo la Pwani imeonyesha kwamba, mahoteli, makanisa, mashirika ya kiserikali na hata mabwenyenye wenye ushawishi mkubwa nchini wamehusika katika unyakuzi ardhi iliyotumiwa na wavuvi.

Mengi ya maeneo ni yale ambayo hutumiwa na wavuvi kuegesha boti zao baada ya shughuli zao au maeneo ambapo wanafaa kujenga mitambo ya kuhifadhi samaki wanaovua.

Ripoti hiyo inajulikana kama ‘Nowhere to Land -The case of grabbed, inaccessible and neglected fish landing sites in Mombasa’ na ilitayarishwa na shirika la Haki Yetu lilikoko jijini Mombasa.

Aidha, ripoti hiyo imesema na kusisitiza kwamba maeneo ya kuegesha boti ambayo awali yalikuwa chini ya ulinzi wa wavuvi sasa hayako tena.

Kulingana na ripoti hiyo maafisa wa lililokuwa baraza la mji wa Mombasa wakishirikiana na maafisa wa wizara ya ardhi walitoa ardhi hiyo ufuoni bila kujali kwamba waliziba barabara.

“Sasa ardhi yote katika ufuo wa bahari iko chini ya watu binafsi na ni vigumu wavuvi kuifikia tena na hivyo basi kukwamiza biashara ya uvuvi kwa asilimia kubwa,” yasema sehemu ya ripoti hiyo.

Inasema kwamba eneo la Kibarani ambalo lilikuwa katika himaya ya serikali kwa miaka 99 sasa iko katika mikono ya makampuni ya kibinfasi.

Eneo la kuegesha boti la Bamburi kulingana na ripoti hiyo, liligawanywa vipande vipande ambavyo vimekuwa vikigawiwa watu wenye ushawishi tangu mwaka wa 1968.

Eneo la uvuvi la Shimanzi kwa sasa liko na takataka nyingi ambazo zinatoka katika lililokuwa jaa la taka la Kibarani na daraja fupi linalounganisha barabara kuu na kampuni moja ya kibinfasi eneo hilo.

“Daraja hilo limekuwa kiini cha masaibu ambayo wavuvi hupitia na mara nyingi boti zao zimekuwa zikiligonga na kuwaletea madhara. Egesho la dau la Tudor pia limenyakuliwa na wavuvi sasa wamesukumwa ndani kabisa ya bahari huku eneo hilo likiendelea kunyakuliwa,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kuzibwa

Aidha ripoti hiyo inasema kwamba eneo la Mji wa Kale ambalo liko na maegesho matano ya wavuvi, sasa limezibwa na shughuli za ujenzi na ni vigumu kuyafikia maeneo hayo.

“Kuna maeneo matano ya uvuvi katika eneo hilo ambayo ni Soko Kuu la Zamani, Mbuyuni, Mabandani, Madobini, na Mudubaah. Hata hivyo, maeneo haya yamenyakuliwa na kujegnwa nyumba za kibinafsi. Baadhi ya maegesho pia yamegeuzwa na kuwa maeneo ya kumwaga taka,” ikasema ripoti hiyo.

“Eneo la uvuvi la Kitanga Juu awali lilikuwa likisimamia maeneo matatu ya uvuvi lakini sehemu mbili kati ya tatu hizo ambazo ni Kwa Kanji na Kwa Skembo zilichukuliwa na mashirika ya serikali,” ripoti hiyo inaongeza.

Katika eneo la Nyali, ripoti hiyo ilisema kuwa takribani maeneo yote ya uvuvi yalijengwa kama mahoteli ya kifahari na hakuna matumaini tena ya kuimarisha shughuli za uvuvi.

Mkurugenzi wa shirika hilo Padre Gabriel Dolan alisema kuwa unyakuzi wa ardhi za wavuvi ni dhuluma ambayo Rais Uhuru Kenyatta anafaa kuingilia kati na kuimaliza kabisa.

You can share this post!

Ruto ahimiza mazungumzo kuhusu utata wa fedha

MWANASIASA NGANGARI: Mlezi wa wanasiasa tajika Pwani

adminleo