• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mipango ya magavana 2022 wakihitimisha mihula ya pili

Mipango ya magavana 2022 wakihitimisha mihula ya pili

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA 21 ambao wanahudumu muhula wa pili wameanza mikakati ya kujipanga kusudi wasibaki katika baridi ya kisiasa baada uchaguzi mkuu wa 2022.

Sababu ni kwamba kulinga na kipengee cha 180 (7) cha Katiba ya sasa magavana hawaruhusiwi kushikilia nyadhifa hizo kwa zaidi ya mihula miwili.

Wanne kuwania urais

Hii ndio maana angalau magavana wanne wametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, kwani wanahisi kuwa hiyo ndio wadhifa wa kipekee wenye hadhi ambayo unashabihiana na wadhifa wanaoushikilia sasa.

Wao ni; Mbw Wycliffe Oparanya (Kakamega), Hassan Joho (Mombasa), Alfred Mutua (Machakos), Amason Kingi (Kilifi) na Kivutha Kibwana (Makueni).

Magavana wanaonekana kupania kufuata nyayo za magavana saba wa zamani nchini Amerika ambao walifaulu kushinda urais. Miongoni mwao ni; George W. Bush, Bill Clinton, Franklin Roosevelt, Jimmy Carter kati ya wengine.

Nyadhifa za juu serikalini

Magavana wengine kama vile, Josephat Nanok (Turkana) na Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Samuel Tunai (Narok), Sospeter Ojaamong’ (Busia) na Salim Mvurya (Kwale) wanaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu 2022 kwa kwa matumaini kuwa watateuliwa katika nyadhifa za juu serikalini. Hii ni endapo Dkt Ruto atafaulu kumrithi Rais Uhuru Kenyatta anayehudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

Naye Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria anasemekana ndiye mdhamini wa chama kipya cha kisiasa cha Civic Renewal Party (CRP) ambacho kilisajiliwa rasmi mwaka jana. Duru zasema kuwa Bw Wa Iraia anapania kutumia chama hicho kubuni miungano ya kisiasa na vyama vingine vikuu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ili angalau asalie kwenye ulingo wa kisiasa.

Kuwania useneta

Lakini Gavana wa Siaya Cornell Rasanga amesema kuwa atawania kiti cha Useneta baada ya James Orengo kudai kuwa anakimezea mate kiti hicho.

Na wengine kama vile James Ongwea (Kisii), Paul Chepkwony (Kericho), Ali Roba (Mandera) na John Nyagarama (Nyamira), Cyprian Awiti (Homa Bay) hawajatangaza waziwazi mipango yao kuelekea 2022, lakini itarajiwa kuwa watatoa misimamo yao uchaguzi mkuu utakapokuwa unakaribia.

Kustaafu katika siasa

Hata hivyo, Gavana wa Embu Martin Wambora ambaye ametangaza kwamba atalikunja jamvi lake la kisiasa na uongozi wa umma baada ya kukamilika kwa kipindi chake cha pili na cha mwisho katika uongozi.

“Baada ya kuhudumu katika siasa kwa miaka 15 nahisi kuwa sasa hiyo imetosha nitastaafu mnamo 2022 baada ya kukamilisha kipindi changu cha pili uongozini,” Bw Wambora akaambia Taifa Jumapili.

Amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Runyenjes kati ya mwaka wa 2003 hadi 2007.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa na kisheria wanasema kando na wadhifa wa urais magavana hao 22 pia wanaweza kuwania nyadhifa zingine za kwenye uchaguzi mkuu ujao isipokuwa ugavana.

“Hakuna sheria inayowazuia magavana hao kuwania kwa mfano nyadhifa za ubunge, useneta na hata udiwani. Kiti kimoja ambacho hawawezi kuwania ni ugavana katiba inawazuia kufanya hivyo,” akasema wakili wa masuala ya kikatiba Bobby Mkangi.

Hata hivyo, wakili huyo ambaye alikuwa mwanachama wa kamati ya wataalamu (CoE) anasema magavana hao wanamezea mate nyadhifa za juu kwa sababu wamezoea mamlaka makuu na udhibiti wa mabilioni ya fedha.

Naye Dkt Alutalala Mukhwana ambaye ni wakili na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anakubaliana na kauli ya Bw Mkangi kwamba magavana hao wako huru kuwania viti vyovyote katika uchaguzi bali sio ugavana.

Uwaziri na ukatibu wa wizara

“Ilivyo sasa wanasema kuwania urais au cheo chochote kile isipokuwa ugavana. Na ikiwa wana hamu ya kuendelea kuhudumia umma, wanaweza pia kuwania viti vya useneta, ubunge na hata udiwani. Wanaweza pia kuwahudumia Wakenya katika nyadhifa za uwaziri na ukatibu wa wizara,” anasema.

Kujiongezea sifa kisiasa

Lakini kulingana na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Herman Manyora magavana wanne ambao wametangaza azma ya kuwania urais wamefanya hivyo ili kujiongezea sifa za kisiasa wala sio kwa lengo la kushinda.

“Haja yao kuu ni kuonekana na wagombeaji wakuu ambao ni Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga ili waweze kupewa nyadhifa za hadhi ya juu katika serikali ijayo. Kimsingi, hawana ushawishi wowote nje ya kaunti zao kuwawezesha kuibua upinzani mkali dhidi ya Raila na Ruto,” anasema Bw Manyora ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

“Ikiwa Raila atawania urais, na dalili zote zinaonyesha kuwa atakuwa debeni, basi Oparanya na Joho watalazimika kujipanga kwa viti vingine vya ngazi za chini” anaongeza.

Hawatakuwa na ushawishi wowote

Na Dkt Mutua na Profesa Kibwana, kulingana na Dkt Manyora, hawatakuwa na ushawishi wowote nje Ukambani na maeneo mengine nchini ikiwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka hatastaafu kutoka ulingo wa siasa.

Lakini Bw Oparanya ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) anashikilia kuwa hayuko tayari kwa kiti chochote kila isipokuwa urais.

“Macho yangu yote yanalenga urais. Nimekomaa kwa siasa za kitaifa. Hii ndio maana wakati huu ninawaomba ndugu zangu Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula na hata kiongozi wa ODM Bw Odinga waniunge mkono,’ anasema mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri wa Mipango katika Utawala wa Rais Mstaafu Moi.

Naye Bw Joho wiki jana alimhakikishia Rais Kenyatta kwamba wakati huu amesitisha siasa ili kutoa nafasi kwa vita dhidi ya ufisadi na utekelezaji wa Agenda Nne za Maendeleo.

“Lakini wakati ukitimu, nitakuwa ulingoni kama ambavyo nimekuwa nikiwaambia Wakenya na haswa Wapwani, kila mara,” akasema.

You can share this post!

JAMVI: Vizingiti vya Ruto ndani ya Serikali

KCB mabingwa wa Kakamega 7s

adminleo