• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MARY MONI: Wakati mwingine sisi waigizaji hatulipwi

MARY MONI: Wakati mwingine sisi waigizaji hatulipwi

Na JOHN KIMWERE

NI kati ya wasanii wengi wa kike ambao wamejifunga nira kuvumisha tasnia ya maigizo hapa nchini.

Anaamini anaendelea vyema kukuza talanta yake anakolenga kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo maana anatamani sana kumpiku mwigizaji mahiri na mzawa wa Marekani, Viola Davis.

Mary Wanjiku Moni ambaye kando na uingizaji ni mwandishi wa filamu na mwanabiashara anayeibukia. Kwenye uigizaji wa filamu anajulikana kama ‘Nuchi’ na kwenye redio anatambulika kama ‘Mama Safi.’

Unajua nini? Kisura huyu anasema tangu utotoni mwake alitamani kuhitimu kuwa mwigizaji mtajika na msanifu.

”Bila shaka kila mwanadamu huwa na malengo fulani nami pia siwezi kuachwa nyuma nimepania kujizatiti kadiri niwezavyo angalau nifanye kweli katika tasnia ya maigizo,” anasema na kuongeza kuwa ni kipaji alichokitambua akiwa mdogo.

Anajivunia kuwa miongoni mwa wasanii ambao hushiriki kipindi cha vichekesho kiitwacho ‘Safi Safi’ ambacho hupeperushwa kupitia redio stesheni ya Redio Mtaani.

Dada huyu alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji miaka sita iliyopita alipojiunga na kundi la Rafiki Mwafrika. Anadai ameamua kutolegeza kamba baada ya kutazama alipotazama filamu ‘Twelve Years A Slave’ aliyoshiriki mwigizaji wa Kenya anayetesa kwenye filamu za Hollywood, Lupita Nyong’o.

”Kusema kazi yake Lupita Nyong’o ametia Wakenya wengi motisha maana wengi tumeamua kujikakamua kwa imani nasi pia tunaweza,” anasema.

Mwigizaji Mary Wanjiku Moni maarufu Nuchi. Picha/ John Kimwere

Kipusa huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa ambazo zimefanikiwa kupeperushwa kupitia kituo cha runinga cha Inooro TV, ikiwamo ‘Wendo Nduri Mihaka,’ Mwihoko,’ zilizozalishwa na Jonvinjo Venture Production bila kuweka katika kaburi la sahau ‘Black Gate TV Series’ iliyotengenezwa na kundi la Rafiki Mwafrika.

Katika uandishi wa Script analenga kujitahidi kwa udi na uvumba angalau kufikia kiwango cha Abel Mutua na Wanuri Kahiu (Wakenya) pia John Logan mzawa wa Marekani. Mrembo huyu anajivunia kuandika filamu kadhaa ikiwamo ‘Black Gate TV Series,’ ‘Wendo Nduri Mihaka,’ ‘Mwihoko’ na ‘Along The Road’- Stori fupi inayopatikana kwenye mtandao wa kijamiii wa Youtube.

Katika mpango mzima binti huyu anayepania kumiliki brandi yake miaka ijayo anasema angependa sana kufanya kazi na Wakenya wenzake kama Nini Wacera na Catherine Kamau ambao walishiriki filamu ‘D Minor,’ ‘Rafiki’ na ‘Nairobi Half Life,’ ‘Plan B,’ mtawalia.

Kwa kuwa wana maigizo wa hadhi ya juu anatamani kushirikiana nao Lupita Nyong’o kati ya walioshiriki filamu za ‘Queen of Katwe,’ na ‘Shuga.’

Pia yupo mzawa wa Nigeria, Genevieve Nnaji filamu zake ambazo humvutia zaidi zikiwa ‘Rising Moon, na ‘Behind Closed Door.’

Anasema waigizaji wengi hasa wanawake hupitia changamoto nyingi ikiwamo nyakati zingine kutolipwa licha ya kufanya kazi. Kadhalika anawaponda maproduza wengi ambao hupenda kushusha hadhi ya wanawake na kuwatamani kushiriki ngono nao ili kuwapa ajira ya kuigiza.

You can share this post!

Nairobi Water yajipanga kurejea ligini

Kuria ajiona kama ‘zawadi’ kwa Wakenya

adminleo