• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Sonko amtaka afisa kujiuzulu kuhusu barabara mbovu

Sonko amtaka afisa kujiuzulu kuhusu barabara mbovu

NA MARY WANGARI

Gavana wa Nairobi Mike Sonko mnamo Jumanne, Julai 23 alimzomea vikali na kutishia kumpiga kalamu mmoja wa maafisa wake wakuu baada ya kupokea malalamishi mitandaoni kuhusiana na hali duni ya barabara jijini.

Gavana alimtaka Kamishna wa Kaunti (CEC) kuhusu barabara Bw Hitan Mijevda pamoja na katibu wake kujiuzulu kufuatia ujumbe kwenye Facebook uliolalamikia kuhusu barabara mbovu jijini Nairobi.

Akijibu ujumbe huo, Bw Sonko alidokeza kwamba kulikuwa na ufisadi uliokuwa ukiendelezwa huku akifichua kwamba mashine za kuziba mashimo katika barabara jijini Nairobi zilinunuliwa zaidi ya miezi 8 iliyopita ilhali hakuna kitu chochote kilichokuwa kimefanywa.

Bosi huyo wa kauti ya Nairobi alimzomea waziri wake akimtaka ama kuwafanyia kazi wakazi wa Nairobi au kujiuzulu na kumkabidhi usukani yeyote anayeweza kufanya kazi.

Alimtaka waziri wake kuhusu barabara kuelezea vilikoenda vifaa vya kutengenezea barabara ikiwemo mashine za kuzibia mashimo barabarani pamoja na kiwanda kipya cha kutengenezea lami kilichonunuliwa miezi 8 iliyopita.

“Viko wapi vifaa vyetu vya kurekebisha barabara ambazo wahandisi wetu walikuwa wakitumia kutengenezea barabara ama umevihodhi ili uwape kazi wanakandarasi wa kibinafsi?

“Ikiwa mmelemewa na kazi mko huru kujiuzulu na kwenda nyumbani. Tuko na wahandisi wengi wachanga wenye nguvu ambao hawana kazi jijini Nairobi,” gavana alifoka.

Bw Sonko alimpa waziri pamoja na katibu wake makataa ya siku 14 ya kutekeleza wajibu wao la sivyo wajiuzulu.

Isitoshe, gavana huyo alidokeza kuhusu mipango ya kupanga upya baraza lake baada ya kugundua ulegevu katika utendakazi miongoni mwa baadhi ya mawaziri wake katika baraza la kaunti.

“Baadhi ya mawaziri huja hapa kama malaika lakini ghfal wanabadilika baada ya kujiunga na mabwenyenye kwa sababu waliletwa hapa na vigogo wao hawawezi kufutwa kazi.

“Ninataka kuwafahamisha leo kwamba sitasita kuwafuta kazi,” alisema.

Haya yanajiri siku mbili tu baada ya Bw Sonko kumteua Bw Charles Kerich kama wa ‘Waziri Mahsusi” na kumtwika jukumu la kusimamia mawaziri wengine katika Baraza la Jiji.

You can share this post!

Meltah Kabiria waimumunya Kawangware United 4-0

Mhubiri wa SDA akatakata mke wa ndugu yake

adminleo