• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Shirika lataka IDP bandia waliopokea fidia wachunguzwe

Shirika lataka IDP bandia waliopokea fidia wachunguzwe

 Na GERALD BWISA

KUNDI linalopigania masilahi ya Wakimbizi wa Ndani kwa Ndani maarufu  kama IDPs wanaitaka Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kuchunguza namna wakimbizi hewa walilipwa fidi ya mamilioni ya fedha.

Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, inaonyesha kuwa fedha zilizolipwa kiholela zilikuwa sehemu ya Sh2.7 bilioni zilizohifadhiwa katika Hazina ya Kitaifa ya Misaada ya Kibinadamu kusaidia waathiriwa wa vurugu za kisiasa na mizozo ya rasilimali.

Katibu wa Mtandao wa IDPs, Raphael Eyanai, ameitaka serikali kuanzisha uchunguzi ili kubaini wakimbizi hewa walionufaika na fedha hizo.

“IDPs 310,000 ambao tayari wanaishi na jamaa zao ndio walifaa kunufaika na malipo hayo. Kundi la kwanza la wakimbizi 83,891 walilipwa Sh50,000 kila mmoja,” Bw Eyanai akaambia Taifa Leo mjini Kitale.

Wizara ya Fedha ndiyo ilipaswa kusimamia hazina hiyo lakini malipo yalifanywa na Kamati Maalumu ya Mashauriano ya Kitaifa (NCCC) chini ya wizara ya Ugatuzi.

Bw Eyanai alidai kuwa IDPs halisi ambao hawajapokea fidia yao wamekuwa wakitapeliwa na baadhi ya watu walio na ushawishi serikali wanaowataka kutoa hongo ili kuwasaidia kupata malipo hayo.

“Kaunti zilizo na visa vingi vya utapeli ni Kisii, Nakuru, Uasin Gishu, Trans Nzoia, Siaya na Kisumu. Tumeripoti visa vingi vya utapeli kwa polisi,” akasema.

Kulingana na shirika hilo, IDPs 310,000 walioathiriwa na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 hajanufaika na fidia hiyo iliyotolewa na serikali wakati wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

“Wengi wa IDPs walionufaika na fidia hiyo ni wale walikuwa wakiishi kwenye kambi za wakimbizi 118 kote nchini. Lakini walioenda kuishi na jamaa zao walisahauliwa,” akasema.

Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC) inayoongozwa na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, inaendelea kukagua ripoti ya Bw Ouko ambayo imefichua kuwa IDPs bandia walipokea fedha za fidia kutoka kwa serikali.

Kamati ya PAC imeandaa orodha ndefu ya maafisa wa serikali watakaohojiwa, akiwemo Katibu wa Wizara ya Fedha Kamau Thugge ambaye sasa anakabiliwa na mashtaka ya ufujaji wa fedha za umma katika mradi wa mabwawa ya Kamwerer na Arror.

Ripoti inaonyesha kuwa majina ya IDPs waliolipwa Sh17.8 milioni katika kaunti 16 yalikuwa yamerudiwa zaidi ya mara mbili.

You can share this post!

Sonko aiga Rais, ateua msimamizi wa shughuli za wizara zote

NGILA: Kongole Microsoft kufadhili vipusa kuboresha kilimo...

adminleo