Makala

NGILA: Kongole Microsoft kufadhili vipusa kuboresha kilimo nchini

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTINE NGILA

TANGAZO la kampuni ya teknolojia ya Microsoft wiki iliyopita kuwa itafadhili kampuni ibuka ya humu nchini inayomilikiwa na wanadada kukuza kilimo linastahili pongezi.

Kampuni hiyo inalenga kuwasaidia Clara Nashipai, Sylvia Achach, Rosianah Musyoka na Bethany Jepchumba kuunda programu moja mwafaka itakayowasaidia wakulima kubashiri mimea inapokaribia kuvamiwa na wadudu na magonjwa.

Awali katika safu hii niliwashangaa mabinti wa humu nchini kwa hulka yao ya kuonekana kusalia nyuma katika uvumbuzi unaoleta maendeleo ya kiuchumi. Lakini sasa ninatabasamu kuona kwamba kampuni gwiji ya teknolojia imewatambua na kuwapa fursa kuongoza mageuzi ya kilimo chetu.

Wanawake hao wanaomiliki ‘The BugSlayers’ wenye ari ya kuzindua programu kwa jina AgRight watasaidiwa na kampuni hiyo kuhakikisha programu yao haina kasoro kama baadhi ya programu za simu za humu nchini ambazo hulemewa kutoa huduma zinazoahidi watumizi.

Uwezo wa teknolojia hiyo wa kuzuia usambazaji wa magonjwa ya mimea na kuenea kwa wadudu, huku ikitoa suluhu kwa matatizo ya wakulima, utalifaa taifa hili hasa wakati huu ambapo tunashuhudia ukosefu wa nafaka muhimu nchini.

Na si kuzuia magonjwa pekee, wanadada hawa wamejipa jukumu la kubashiri wakati mazao yatakomaa na kuvunwa huku pia ikiwaunganisha wakulima na wanunuzi. Itafuatilia shughuli zote za shambani na kuwazima wezi wa mazao.

Kwa muda mrefu, sekta ya teknolojia nchini imetawaliwa na wanaume ambao ingawa wamevumbua mbinu za kuvumisha uchumi, wamesahau kuunda teknolojia za kuwafaa wanawake. Wao husahau kuwa wanawake ni nguzo muimu ya jamii, na hata teknolojia wanazounda hutumiwa na watu wa jinsia zote.

Na sasa ni jambo la kutia moyo kuwaona wanawake wakiwa katika mstari wa mbele kuondolea wakulima wetu changamoto katika uwekezaji wao katika dhamira kuu ya kuangamiza njaa nchini.

Iwapo mkulima atang’amua kuwa wiki mbili zijazo kuna ugonjwa au wadudu watakaovamia mimea yake, basi atachukua hatua mapema, kuliko kusubiri kuanza kuona dalili za magonjwa kwenye majani ya mimea.

Chakula kingi hupotea kutokana na mbinu mbovu za kupanga, kupalilia, kuzuia magonjwa na kuvuna. Lakini ujio wa teknolojia hii utatusaidia kupunguza idadi ya watu wanaoangamia kutokana na njaa.

Heko kwa vipusa hao wanne, lakini sasa wanahitaji kupigwa jeki vilivyo na Wizara ya Kilimo na ile ya Teknohama.