• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wanafunzi waliopanga kumuua mwenzao kwa sumu wafukuzwa shuleni

Wanafunzi waliopanga kumuua mwenzao kwa sumu wafukuzwa shuleni

Na PIUS MAUNDU

WANAFUNZI watatu ambao walikuwa wakipanga kumtilia sumu mwenzao katika Shule ya Wasichana ya Makueni kuhusiana na mzozo dhidi ya mvulana walifukuzwa shuleni Jumatano, baada ya mpango wao kutibuliwa.

Wanafunzi hao wa kidato cha pili na ambao wana miaka 15 walikuwa wameshirikiana kumtilia mwenzao wa darasa hilo sumu katika chakula, baada ya kuiba kemikali katika maabara ya shule.

Hata hivyo, naibu wa mwalimu mkuu shuleni humo Dorcas Nzioka alisema kuwa mpango wao ulijulikana mnamo Alhamisi, baada yao kukosana kuhusu ni yupi angetia kemikali hiyo katika chakula.

Kulingana na kamanda wa polisi eneo la Makueni Timothy Maina, wanafunzi hao walipokosana kuhusu yupi aliyefaa kutia sumu hiyo walianza kuzomeana, mmoja wao alifahamisha kiranja kuhusu kiini cha mzozo, naye kiranja akaambia walimu.

Wanafunzi hao wanadaiwa kupanga kumtilia sumu mwenzao kama mbinu ya kumuadhibu, kwa kuchukua mpenzi wa mmoja wao. Mvulana husika ni mwanafunzi katika shule jirani ya Makueni Boys.

Bi Nzioka aliripoti kisa hicho kwa polisi, ambao walifika shuleni humo na kuwakamata wanafunzi hao.

Polisi, hata hivyo, hawakuwazuilia wanafunzi hao seli, badala yake wakiwarejesha shuleni ili waadhibiwe kulingana na sheria za shule.

Bi Nzioka jana alisema kuwa shule inashughulikia kesi hiyo, japo hakutoa maelezo zaidi kuihusu.

Hata hivyo, mtu aliye na ufahamu kuhusu jinsi kesi yenyewe inaendeshwa alifahamisha Taifa Leo kuwa usimamizi wa shule uliwatuma nyumbani wanafunzi hao. Hata hivyo, mtu huyo hakutaka kutajwa kwa kuwa haruhusiwi kutoa habari kwa vyombo vya habari.

You can share this post!

Pendekezo vijana wasio na kazi wapewe Sh48,000 na serikali

Maafisa wa mbuga wadai Sh1.9 milioni zilizopotea zilimezwa...

adminleo