Wanasayansi waunda dawa ya kumaliza kansa

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WANASAYASI wametengeneza dawa ambayo ina uwezo wa kuupa mwili nguvu zaidi kupigana na ugonjwa wa saratani.

Wanasayansi hao kutoka Amerika wametengeneza dawa hiyo ambayo ina uwezo wa kupenyeza katika uvimbe unaosababishwa na saratani na kuua uwezo wake, hivyo ikiponya ugonjwa huo hatari.

Walifanya utafiti kwa kutumia panya, wakiitumia dawa hiyo pamoja na ile ya CAR-T ambayo imekuwa ikitumiwa kutibu ugonjwa huo, japo bila mafanikio kwa wagonjwa wa saratani za maini na matiti.

Dawa hiyo ilimaliza uvimbe katika wanyama hao, na pia iliendelea kuwa na uwezo wa kuwawezesha panya hao kupigana na uvimbe kwa miezi, baada ya kudungwa dawa yenyewe.

Wanasayansi hao walisema dawa hiyo inasaidia kutengeneza seli ambazo zinagundua saratani na kuivamia punde tu inapoingia mwilini.

Watafiti hao walisema wanapanga kujaribu uwezo wa dawa hiyo kwa binadamu, ndani ya kipindi cha mwaka.

Utafiti huo ulifanywa na chuo kikuu cha teknolojia, Massachusetts ukiongozwa na mwanasayansi Leyuan Ma wa kutoka Taasisi ya utafiti kuhusu Saratani ya Koch.

“Kwa kuongeza dawa hiyo kwa ile ya CAR-T, uwezo wa kutibu Saratani ulizidi. Iliipa nguvu kutibu zaidi ya nusu ya Wanyama,” akasema Prof Darrell Irvine.

Matibabu ya CAR-T yamekuwa yakihusisha kuchukua seli fulani za kukinga mwili kutoka mwilini mwa mgonjwa wa Saratani, kisha kuziweka katika maabara na kuzifanya kukinga mwili kutokana na saratani kwa kuweka protein, kabla ya kuzirejesha.

Lakini wanasayansi waligundua kuwa matibabu ya CAR-T japo, yalisaidia baadhi ya wagonjwa haikuwa ikifanya kazi kwa wagonjwa wenye uvimbe, hasa kwenye ini ama matiti.

Waliamua kuzipa nguvu seli za T, kama mbinu ya kuziwezesha kupigana na uvimbe wa ndani ya mwili, na kufanya seli hizo za T, kuzalishwa kwa wingi.

“Utafiti wetu ulikuwa kuwa ukiinua seli za T kwa kutumia CAR, zitafanya kazi zaidi,” akasema Dkt Irvine.

Baada ya majaribio ya matibabu hayo kwa panya, panya hao waliongeza idadi ya seli za T ndani ya kipindi cha wiki mbili pekee kwa asilimia 60, mbali na uvimbe katika matiti na ini kumalizwa.

Matibabu hayo aidha yalisaidia kuzuia uvimbe kuwahi kutokea tena.

Siku 75 baada ya kupewa matibabu hayo, wanasayansi walijaribu kuwadunga panya seli zenye chembechembe za Saratani, lakini zilimalizwa mara moja, kutokana na kuimarika kwa seli za T, ambazo ni askari wa mwili, kuulinda kutokana na Saratani.

Panya hao aidha waliweza kupigana na uvimbe wowote ambao ulijaribu kuwekwa milini mwao.

“Tukiwachukua Wanyama ambao wanaonekana kupona na kujaribu kuwaweka seli zenye uvimbe, wanazipiga kutoka milini,” akasema Dkt Irvine.

Habari zinazohusiana na hii

SARATANI WATUTAKIANI?