Habari Mseto

Jopokazi la kuimarisha ubora cha chakula labuniwa

July 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

Serikali imeunda kamati inayojumuisha wadau mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa sheria kuhusu ubora wa chakula huku sekta ya chakula nchini ikiyumbishwa na visa tele vya ukiukaji sheria.

Akizungumza na wanahabari mnamo Jumatano, Julai 24 baada ya mkutano wa faragha na kamati hiyo uliondaliwa jijini Nairobi, Katibu Mkuu Idara ya Mifugo Bw Harry Kimutai alisema kamati hiyo itabuni mpango wa utekelezaji utakaosambazwa katika kaunti zote.

“Mpango huo wa utekelezaji utaanzia Nairobi kwa sababu ya nafasi yake na kisha usambazwe katika kaunti zote. Lengo letu ni kuwang’oa wanafanyabiashara wanaoendeleza vitendo haramu katika sekta ya chakula,” alisema Bw Kimutai.

Kamati hiyo itakayoongozwa na Katibu katika Idara ya Mifugo na Uvuvi, Kello Harsama kama mwenyekiti wake, itajumuisha mashirika ya kiserikali na yale ya kibinafsi na italenga bidhaa zote za chakula.

Bw Kimutai pia alidokeza kwamba serikali inabuni mpango thabiti ambapo wafanyabiashara wote katika seka ya chakula walio na leseni watahitajika kujithibiti kibinafsi kinyume na kungoja kukaguliwa na maafisa wa serikali.

“Tunataka wauzaji vyakula kuanza kujisimamia wenyewe kisheria ili tunapotelekeza sheria wasilalamike kwamba hatutaki wafanye biashara. Tutalenga wafanyabiashara walio na leseni.

“Tunataka wajue ni wajibu wao wa kuhakikisha kwamba vyakula wanavyouzia umma ni salama Tatizo ambalo limekuwapo ni kwamba wafanyabiashara mara tu wanapopata leseni wao hulegea na kusubiri hadi watakapokaguliwa na maafisa wa serikali,” alisema.

Aliongeza kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wafanyabiashara watakaopatikana wamekiuka sheria ikiwemo kupokonywa leseni na kupigwa marufuku kufanya biashara yoyote inayohusu chakula nchini.

Kulingana na Katibu Mkuu huyo wajibu wa serikali sasa utakuwa tu kufanya ukaguzi baada ya kipindi fulani cha muda huku wafanyabiashara wakihitajika kuwasilisha ripoti kwa serikali na umma kuhusu mikakati ambayo wameweka ili kuhakikisha bidhaa zao ni salama.

“Wafanyabiashara watakuwa wakiwasilisha mipango waliyo nayo katika kuhakikisha usalama wa bidhaa zao za vyakula. Pia watahitajika kufahamisha umma aina ya chakula wanachouza, kemikali wanazotumia kupakia na kuhifadhi chakula hicho na mambo mengine,” alisema.