• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Kashfa zatia doa uteuzi wa mawaziri

Kashfa zatia doa uteuzi wa mawaziri

Na VALENTINE OBARA

ONGEZEKO la mawaziri wanaoondoka mamlakani katika utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, limeibua maswali kuhusu mambo anayozingatia wakati anapochagua mawaziri wake pamoja na naibu wake, Dkt William Ruto.

Tangu serikali ya Jubilee ilipoingia mamlakani katika mwaka wa 2013, idadi ya mawaziri waliosimamishwa kazi au kujiuzulu imefika wanane.

Hii ni baada ya Rais Kenyatta kufanya mabadiliko kwenye baraza lake jana na kumwondoa Bw Henry Rotich kutoka kwa wizara ya fedha. Bw Rotich anakumbwa na kesi ya ufisadi kwa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer, yaliyo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Kiongozi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, alidai Bw Rotich pamoja na washukiwa wengine 27 walisababisha gharama ya ujenzi wa mabwawa hayo kupanda kutoka Sh46 bilioni hadi Sh63 bilioni kwa njia za kilaghai.

Wakili Ahmednasir Abdullahi alisema wanaopaswa kulaumiwa kwa doa linaloingia baraza la mawaziri mara kwa mara ni Rais na naibu wake kwa sababu wao ndio hushirikiana kuchagua mawaziri.

“Ukiajiri watu waliohitimu, kwa misingi inayostahili, watatekeleza kazi zao ifaavyo. Lakini ukiajiri watu wenye rekodi mbaya, hufai kulia wala kulalamika wakati wanapopanda daraja katika utovu wa maadili,” akasema.

Mnamo Machi 2015, Rais Kenyatta aliwaagiza mawaziri watano wang’atuke mamlakani kwa muda baada ya wizara zao kuhusishwa sana na sakata za ufisadi.

Walijumuisha aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Bi Charity Ngilu ambaye sasa ni Gavana wa Kitui, Bw Felix Koskei (Kilimo), Bw Michael Kamau (Miundomsingi na Uchukuzi), Bw Davis Chirchir (Kawi na Petroli) na Bw Kazungu Kambi (Leba na Huduma za Kijamii).

Mwaka huo huo, aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Bi Anne Waiguru ambaye sasa ni Gavana wa Kirinyaga, alijiuzulu kufuatia shinikizo kali kutoka kwa wakosoaji wa serikali walioongozwa na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Walimkashifu kwa sakata za ufisadi zilizokumba Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) ambapo ilidaiwa Sh790 milioni zilipotea.

Mapema mwaka huu, Bw Rashid Echesa alisimamishwa kazi ya uwaziri katika Wizara ya Michezo, ingawa serikali haijawahi kueleza sababu zilizopelekea hatua hiyo kuchukuliwa.

You can share this post!

Sonko ampa kazi dadake Raila

Ajisaliti kuweka benki mamilioni ya pesa za wizi kila siku

adminleo