• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Nyumba ya Oparanya ya Sh70m yatengewa Sh10m zaidi

Nyumba ya Oparanya ya Sh70m yatengewa Sh10m zaidi

NA BENSON AMADALA

SERIKALI ya Kaunti ya Kakamega imetenga Sh10 milioni kwenye bajeti yake ya mwaka wa kifedha 2019/20 kukamilisha ujenzi wa makazi rasmi ya Gavana Wycliffe Oparanya katika eneobunge la Likuyani.

Ujenzi wa nyumba hiyo itakayogharimu Sh70 milioni kwa jumla, umekuwa ukitengewa fedha kwenye bajeti tangu mwaka wa 2013/14 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu.

Kulingana na Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala katika kaunti hiyo, Dkt Beatrice Sabana, pesa zilizotengewa mradi huo mwaka huu zitatumika kununua samani ili kuhakikisha mazingira ya makazi hayo yanaafiki hadhi inayostahiki na kurekebisha sehemu mbalimbali.

Dkt Sabana pia aliondolewa kaunti hofu kuhusu uwepo wa utata kuhusu hati ya kumiliki ardhi ya shamba ambalo makazi hayo yamejengwa, akisema suala hilo tayari limeshughulikiwa.

“Makazi hayo yamejengwa katika ardhi ya serikali na kile ambacho kimekuwa kikiendelea ni ukamilishaji wa mchakato wa kupokea hatimiliki na sasa hilo limetimizwa,’’ akasema Dkt Sabana.

Hofu kuhusu hatimiliki hiyo iliibuliwa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye ripoti ya mwaka jana ya kifedha, ambapo Bw Edward Ouko alidai kaunti haikuwasilisha cheti hicho wakati wa ukaguzi wa stakabadhi zake.

Bw Ouko kupitia ripoti yake pia alieleza kwamba hakuna habari zozote zilizowasilishwa kuthibitisha kwamba mradi huo uliafikiwa kupitia ushirikishaji wa umma.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kwa afisi ya Bw Ouko, nambari ya kandarasi ya ujenzi ilikuwa CGKK/1617002 na makazi yalikuwa yakijengwa katika eneobunge la Lugari.

Hata hivyo, habari zilizochapishwa kwenye tovuti ilionyesha kwa nambari ya kandarasi ya ujenzi ilikuwa CGK/OG/2015/2016001 na makazi hayo yalikuwa yakijengwa eneobunge la Likuyani.

Dkt Sabane alisema makazi hayo yamekamilika na ni mambo machache pekee yaliyosalia kabla ya shughuli zote za ujenzi kusitishwa na yawe tayari kutumika na gavana.

Bw Oparanya amekuwa akiendesha masuala ya kaunti kutoka nyumbani kwake Emabiole, Kaunti ndogo ya Butere kutokana na ukosefu wa makazi rasmi ya gavana mjini Kakamega.

Bunge la kaunti nalo lilipendekeza wizara ya Dkt Sabane ikamilishe ujenzi wa makazi ya gavana haraka iwezekanavyo ili yaanze kutumika rasmi na kinara wa kaunti.

You can share this post!

Serikali sasa yaongeza muda wa raia kupata paspoti mpya

ODM yapuuzilia mbali juhudi za ‘Punguza Mizigo’

adminleo