Mbunge ahimiza viongozi wazingatie maendeleo badala ya siasa 'duni'
Na LAWRENCE ONGARO
VIONGOZI wamehimizwa kujishughulisha na maendeleo na kuachana na siasa ambazo hazina msingi.
Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega, ambaye yuko katika kamati ya bunge kuhusu viwanda, alisema Alhamisi viongozi wanastahili kuzingatia ajenda nne kuu za serikali ili Rais Uhuru Kenyatta afanikiwe kuacha msingi dhabiti kimaendeleo.
“Wakati kama huu serikali inastahili kubuni viwanda vidogo vitakavyosaidia vijana wetu kupata ajira. Wakati kama huu hatufai kuagiza viberiti kutoka nchi za nje,” alisema Bw Kega.
Alisema Kenya inastahili kujitegemea kwa kujenga viwanda vingi ili kuajiri vijana wengi ambao hawana ajira kwa sasa.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kiwanda kipya cha Bidco Industrial Park ambacho ujenzi wake unakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh10 bilioni.
Alisema la muhimu kwa wakati huu ni kupunguza ada ya umeme hadi kiwango cha asilimia 50 ili viwanda viweze kupiga hatua zaidi kwa urahisi.
Kuhusu siasa za nchi, alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Noordin Haji na Mkuu wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai Bw George Kinoti wanastahili kupewa nafasi kuendesha kazi yao bila kuingiliwa na yeyote.
“Inashangaza kusikia viongozi fulani wakidai kuwa watu wao ndio wanaonewa kuhusu ufisadi,” alisema Bw Kega.
Aliwataka wasubiri hadi uchunguzi utakapokamilika kwa washukiwa na baadaye wapelekwe mahakamani ili nao wajitetee.
Alisema mwananchi wa kawaida ‘Wanjiku’ anataka kuona maendeleo katika eneo lake na sio kupigiwa siasa kila mara.
“Wanasiasa wanastaahili kukoma kuzungumza kuhusu makabila yao kwani matamshi kama hayo yanaweza kuwachochea wananchi na kuzua taharuki nchini,” alisema mbunge huyo.
Alisema iwapo kila kiongozi atajihusisha na maendeleo bila shaka mwananchi wa kawaida atanufaika pakubwa na nchi itapiga hatua kubwa kimaendeleo.