• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Kanisa nalo laweka kibanda katika uwanja wa maonyesho Kisumu

Kanisa nalo laweka kibanda katika uwanja wa maonyesho Kisumu

Na MARY WANGARI

KANISA Katoliki mjini Kisumu halikuachwa nyuma Alhamisi pale liliweka kibanda katika Maonyesho ya Kilimo yaliyong’oa nanga katika mtaa wa Mamboleo mnamo Jumatano, Julai 24, 2019.

Hatua hiyo imeibua hisia mbalimbali miongoni mwa watu; hasa waliohudhuria maonyesho hayo.

Kwa miaka mingi, maonyesho hayo ya kilimo yanayofanyika kila mwaka, yamehusishwa na watangazaji bidhaa kutoka sekta ya kilimo.

Aidha, tamasha hiyo imekuwa kivutio kikuu kutokana na vituo mbalimbali vya watoto kuchezea na sehemu za burudani.

Maonyesho hayo ya Kisumu vilevile yamezidi kujitwalia umaarufu kila mwaka kutokana na hatua yake ya kuandaa tamasha ya Omega One inayowavutia wapenda burudani na muziki wa kidunia kutoka pande zote za nchi.

Hata hivyo, kituo cha Kanisa la Katoliki katika maonyesho ya mwaka 2019 kimevutia watu wengi kiasi cha kusababisha msongamano na wakati uo huo kuibua hisia tofauti.

Kasisi Samuel Nyataya, ambaye ni Mwelekezi wa Caritas katika dayosisi ya Kisumu hata hivyo alishikilia maoni tofauti akisema kanisa hilo linatoa mtazamo jumuishi kuhusiana na masuala ya maisha.

“Kuwepo kwetu hapa si jambo geni. Swali sahihi ambalo watu wangekuwa wakiuliza ni kwa nini hatuko hapa?” alisema Nyataya.

Kasisi Nyataya anayeongoza idara ya maendeleo ya Kanisa Katoliki mjini Kisumu alisema kanisa hilo katika miaka iliyopita liliweka kituo kwenye uwanja huo na kukaa mbali kwa sababu zisizojulikana.

Wakatoliki, wengi wao wakiwa watangazaji bidhaa uwanjani humo walifurika katika kituo hicho wakati wa kila kipindi cha mapumziko ya chamcha ili kuimba pambio na kushiriki katika misa takatifu zinazoongozwa na makasisi wa Kikatoliki.

“Wanaopanda kwa machozi wataimba watakapovuna. Lau taswira kutoka juu ingewasilishwa mtu angebaki akishangaa mkusanyiko huu mdogo ni nini?” alitania Kasisi.

Akaongeza: “Hata hivyo, hii inawakilisha picha halisi ya jinsi ulimwengu ulivyogeuka. Kila kiumbe anajishughulisha na maisha yake akisahau sisi ni vyombo tu vya udongo vinavyoweza kuvunjika.”

You can share this post!

Idara maalumu yaundwa kukabiliana na changamoto za ukame...

Mbunge Ken Okoth wa Kibra afariki

adminleo