• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kenya na Tanzania kufufua uhasama, mara hii kwa CHAN

Kenya na Tanzania kufufua uhasama, mara hii kwa CHAN

Na JOHN ASHIHUNDU

Vita vipya kati ya Harambee Stars na Taifa Stars ya Tanzania vinatarajiwa kufufuka hapo kesho Jumapili timu hizo zitakapokutana katika pambano la mchujo wa michuano ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wanocheza ligi za nyumbani (CHAN).

Timu hizi zinakutana mwezi mmoja tu baada ya kukabiliana nchini Misri katika mechi ya AFCON ambapo Harambee Stars ilitoka nyuma na kushinda 3-2.

Harambee Stars ambao wataondoka nchini Jumamosi asubuhi watakuwa wakitafuta ushindi wa pili mfululizo, wakati Tanzania wakipigania kulipiza kisasi kufuatia kichapo cha Misri. Mshindi baada ya mikondo miwili atakutana na Sudan katika raundi ya mwisho ya kufuzu kwa fainali za CHAN.

Wakati Tanzania ikijivunia karibu kikosi chake kizima kilichocheza nchini Misri, Harambee Stars itaingia uwanjani bila wachezaji wake sita.

Lakini licha ya kutokuwepo kwa nyota hao, nahodha wa KCB, Michael Kibwage ameeleza matumaini makubwa ya Harambee Stars kuandikisha matokero mazuri katika mechi hiyo.

“Tunatarajia vijembe vya kila aina jijini Dar es Salaam kesho Jumapili lakini baadhi yetu tumezoea matusi ya mashabiki,” alisema nyota huyo wa zamani wa AFC Leopards.

“Tumejiandaa vyema na tuko tayari kwa upinzani wowote, na ningependa kuwahakikishia mashabiki wetu kwamba tutacheza vizuri na kuwafurahisha,” aliongeza.

Akizungumza na waandishi jana, kocha Sebastien Migne alisema vijana wake wako katika hali nzuri, isipokuwa hakueleza alipo mshambuliaji matata, John Avire wa Sofapaka.

Kwa upande mwingine, kocha wa muda wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije ambaye pia ndiye mkufunzi wa klabu ya Azam ameeleza matumaini makubwa ya wenyeji kupindua matokeo ya AFCON dhidi ya Kenya.

“Tulianza maandalizi yetu vyema, na kila mchezaji ameonyesha juhudi mazoezini na wote wako tayari kwa kibarua cha kesho (Jumapili),” alisema.

“Kwetu, kila mechi ni ngumu, lakini hii ni mechi ambayo lazima tushinde, kwa sababu ni maondoano. Ukipoteza, uko nje, hatukubali kushindwa. Kenya ni timu ngumu, lakini tutajaribu kucheza vizuri tukilenga ushindi,” aliongeza.

Ndiyiragije alipewa jukumu hilo baada ya Emmanuel Amunike kuagana na Shirikisho la Soka Tanzania (TTF) kufuatia matokeo duni katika michuano ya AFCON.

You can share this post!

TAHARIRI: Saratani: Hali yazidi kutisha

MWANAMKE MWELEDI: Ukakamavu ulimpa shavu serikalini

adminleo