Wandani wa Ruto wawaka, walaani vita dhidi ya ufisadi
Na WANDERI KAMAU
WASHIRIKA wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto walichemka vikali Ijumaa, wakidai kile walichotaja kama kukosekana kwa usawa kwenye vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya.
Wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Nelson Koech (Belgut), Hilary Kiplagat (Kipkelion Magharibi), Cate Waruguru (Laikipia) kati ya wengine, walisema wahusika wakuu wa sakata zote za ufisadi wanapaswa kukabiliwa vikali ili kurejesha imani kwenye kampeni hiyo.
Wakihutubu kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Maendeleo wa eneobunge la Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu, wabunge hao walisema vita hivyo havipaswi kukitwa tu katika mabwawa ya Arror na Kimwarer, ilhali kuna fedha nyingi zilizopotea katika ujenzi wa mabwawa mengine, ulipaji fidia katika shamba tatanishi la Ruaraka na Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).
“Washukiwa wote wa ufisadi wakabiliwe vikali, bila ubaguzi wowote. Hilo ndilo pekee litarejesha imani ya Wakenya kuhusu vita hivyo,” akasema Bw Sudi.
Walidai kuna uonevu kuhusu kukamatwa na kushtakiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich, Katibu Kamau Thugge na maafisa wengine katika wizara hiyo kuhusu utoaji zabuni za ujenzi wa mabwawa hayo mawili.
Bw Rotich na Dkt Thugge walikamatwa Jumatatu na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kutozingatia sheria za utoaji kandarasi kwenye sakata hiyo, kufuatia agizo lililotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.
Kupoteza pesa
Inadaiwa kwamba, serikali ilipoteza karibu Sh63 bilioni kwenye sakata hiyo, baada ya kampuni ya CMC di Ravenna kutoka Italia kulipwa fedha hata kabla ya kuanza ujenzi huo.
“Ni lazima washukiwa wote wa ufisadi wakamatwe, akiwemo Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi kuhusiana na sakata ya ulipaji fidia wa ardhi tata ya Ruaraka. Hilo ndilo pekee litatudhihirishia kwamba Bw Haji amejitolea kupigana na ufisadi,” akasema Bw Sudi.
Walidai Bw Haji amekuwa akikwepa kumkamata Dkt Matiang’i, licha ya kukabidhiwa ripoti kuhusu uchunguzi wa sakata hiyo.
“Tunashangaa kuhusu kutokamatwa kwa Dkt Matiang’i, ilhali ripoti za uchunguzi wa sakata hiyo zimo na DPP mwenyewe, Idara ya Upelelezi wa Mashtaka ya Jinai (DCI) na Bunge la Seneti,” akasema Bw Kiplagat.
Bw Koech alisema kuwa Bw Haji anapaswa kuharakisha kukamatwa kwa washukiwa wote wa ufisadi, ikizingatiwa alichukua miezi mitatu pekee kumaliza uchunguzi kuhusu sakata ya mabwawa hayo.