Maoni ya wananchi kuhusu kamari
BERNARD ROTICH na WYCLIFF KIPSANG
WANANCHI wametoa maoni mseto kuhusu michezo ya kamari, baadhi wakitaka sheria zilegezwe huku wengine wakipendekeza masharti makali yanayolenga kudhibiti sekta hiyo.
Masharti hayo yanahitaji wawekezaji wa kigeni kushirikiana na Wakenya kabla ya kuanzisha kampuni za kamari.
Kamati ya Bunge kuhusu Michezo, Utalii na Utamaduni, imekuwa ikizunguka katika maeneo mbalimbali nchini kukusanya maoni ya Wakenya kuhusiana na mswada mpya unaolenga kudhibiti michezo ya kamari.
Mswada huo unalenga michezo ya kamari inayofanyika mitandaoni ambapo washiriki wakuu ni vijana.
Wakizungumza walipofika mbele ya kamati hiyo, wengi wa wakazi wa mjini Eldoret waliwataka wabunge kuweka masharti makali yatakayopunguza idadi ya vijana wanaocheza kamari.
“Vijana wa nchi hii wamepotoka na sasa wanapoteza fedha nyingi kucheza kamari. Wakati umewadia kuweka sheria kali ambazo zitazuia wengi wao kushiriki. Katika siku za usoni tutakuwa na vijana wazembe wasioweza kufanya lolote,” akasema Bw Kibiwott Arap Too, mkazi wa Eldoret.
Lakini Bw Kipkemoi Boit aliwasihi wabunge wasipige marufuku kamari kwani kuna baadhi ya watu wamenufaika.
“Nilikuwa nafanya biashara ya kamari lakini sasa nimelazimika kufunga maduka yangu na vijana zaidi ya 30 wamepoteza kazi na familia zao zinahangaika,” akasema Bw Boit.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw Victor Munyaka alisema mswada huo unalenga kuwanusuru vijana dhidi ya uraibu wa kamari.
“Mswada huu unalenga kudhibiti matumizi ya simu na vifaa vingine vya mawasiliano katika kucheza kamari ambayo imeumiza vijana wengi,” akasema Bw Munyaka ambaye pia ni mbunge wa Machakos Mjini.
“Sheria kuhusu kamari inayotumika sasa ina mapengo mengi ambayo tunalenga kuziba kuifanyia mabadiliko,” akasema.
Kulingana na Bw Munyaka, michezo ya kamari kupitia mitandaoni inasaidia kampuni za pata potea kuhepa kulipa ushuru kwa sababu ni vigumu kwa serikali kufuatilia mapato.