• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
GUMZO LA SPOTI: Real Madrid yamzuia Bale kuenda China

GUMZO LA SPOTI: Real Madrid yamzuia Bale kuenda China

Na MASHIRIKA

TUMAINI la Gareth Bale kutafuna mabilioni ya China limezimwa na waajiri wake Real Madrid ambao kwa sasa wamesema watamdumisha ugani Santiago Bernabeu.

Bale, 30, alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki.

Mapema wiki jana, kocha Zinedine Zidane aliungama kuwa Bale alikuwa pua na mdomo na kuagana na Real, na kwamba kuondoka kwake ni jambo ambalo lingeleta nafuu kubwa ugani Bernabeu.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, maamuzi ya Real kuzuia uhamisho wa Bale katika dakika za mwisho yalichochewa na mambo mawili.

Mosi, walitaka Suning walipie ada ya kumsajili nyota huyu ambaye angali na miaka mitatu kwenye mkataba wake na Real.

Pili, ni jeraha litakalomweka nje winga Marco Asensio kwa kipindi kirefu katika msimu wa 2019-20.

Kukosekana kwa Asensio na Dani Ceballos aliyetua Arsenal kwa mkopo kunawaweka Real katika ulazima wa kuendelea kuyategemea maarifa ya Bale aliyejiunga nao mnamo 2013 baada ya kushawishiwa kubanduka kambini mwa Tottenham Hotspur kwa kima cha Sh11 bilioni.

Mataji

Anajivunia kuwashindia Real mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), moja la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), moja la Copa del Rey, matatu ya Uefa Super Cup na matatu ya Kombe la Dunia.

Aliwafungia Real mabao matatu na penalti moja katika fainali nne zilizopita za UEFA na hivyo kuwanyanyulia ufalme mnamo 2014, 2016, 2017 na 2018.

Wepesi wa kupata majeraha mabaya ni jambo lililomwezesha kuwasakatia Real jumla ya mechi 79 pekee katika kipindi cha misimu minne iliyopita.

You can share this post!

Morans walakiwa kishujaa baada ya kutia fora vikapuni

BURIANI LABOSO: Saratani sasa janga la kitaifa

adminleo