• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Askofu Ng’ang’a motoni tena

Askofu Ng’ang’a motoni tena

Na WAIKWA MAINA

WAUMINI wanaohusishwa na kanisa la Neno Evangelism la Askofu James Nga’ang’a anayezingirwa na utata, walivamia kanisa lililojitenga nao mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, mnamo Jumanne asubuhi.

Kundi hilo lililodai kwamba lilikuwa limetumwa na Askofu Ng’ang’a, lilivamia kanisa la Reformed Neno Gospel Ministry alfajiri na kuharibu ua na sehemu za kuta zilizojengwa kwa mabati ili kuweza kuingia.

Kisha wafuasi hao walipakia mali ya kanisa hilo vikiwemo vifaa vya muziki, viti, meza, vitambaa vya meza miongoni mwa vitu vingine katika lori lilokuwa limeegeshwa nje.

Msimamizi wa kanisa hilo, Pasta Amos Gitau, aliambia Taifa Leo kuwa wamekuwa wakiandamwa na Pasta Ng’ang’a bila kuwepo sababu za kimsingi.

“Askofu Ng’ang’a anafahamu vyema sisi si wa kanisa lake. Hakuchangia hata shilingi kufadhili kanisa hili na hajui tulivyopata ardhi hii,” alisema Pasta Gitau.

Kundi hasimu lililotumwa kutoka Nairobi lilishindwa kutoa nakala za korti au barua yoyote kutoka kwa Askofu Ng’ang’a kuthibitisha kwamba anamiliki kanisa hilo na mali aliyotaka kuchukua.

Naibu Kamanda wa Polisi katika eneo la Nyandarua, Bi Frorence Karimi, alisema maafisa wake wanachunguza kisa hicho, huku wakilinda mali ya kanisa.

“Tulilazimika kufungia mali ya kanisa katika kituo cha polisi ili kuzuia uharibifu. Maafisa wetu wameanza kuchunguza tukio hili,” akasema Bi Karimi.

Mmoja wa waumini, Bi Agnes Kagendo, alisema walilazimika kujitenga na kanisa la Neno Evangelism miaka miwili iliyopita kutokana na alichodai kuwa mienendo ambayo haikuwaridhisha.

“Askofu Ng’ang’a hamiliki chochote hapa. Tulijenga kanisa hili. Tulileta fanicha na kila kitu unachokiona kupitia michango na harambee. Tunazo risiti za kuthibitisha kuwa mali yote iliyo katika kituo cha polisi ni yetu,” akasema Bi Kagendo.

Askofu Ng’ang’a amekuwa akikabiliwa uasi miongoni mwa baadhi ya viongozi wa kanisa lake, na kuna wakati aliponaswa akiwakemea vikali.

You can share this post!

Mswada wa Punguza Mizigo wapata pigo mahakamani

Shule 332 za udereva kufungwa kote nchini

adminleo