Habari MsetoSiasa

Kampuni za kamari ziruhusiwe kuendelea kuhudumu – Maseneta

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wameitaka serikali kuziruhusu kampuni za kamari ambazo leseni zao zilifutiliwa mbali kuendelea na shughuli zao huku suala la iwapo zimekuwa zikilipa ushuru au la likishughulikiwa na wadau katika sekta hiyo.

Wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Masuala ya Haki ya Kibinadamu waliisuta Bodi ya Kudhibiti Michezo ya Kamari na Bahati Nasibu (BCLB) kwa kudharau agizo la mahakama lililositisha hatua hiyo dhidi ya kampuni 27 za kamari.

“Isitoshe, hatua hiyo ilichukuliwa kabla ya kutatuliwa kwa mzozo kuhusu ushuru ambao uko mbele ya Jopo la Kutatua Mizozo kuhusu Ushuru (TAT). Huu ni ukiukaji wa sheria na haki za kampuni husika ambazo zinawaajiri Wakenya wengi, haswa vijana,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Samson Cherargei.

Alisema hayo jana wanachama wa kamati hiyo walipokutana na wakuu wa kampuni nne za kamari miongoni mwa 27, kusikiza malalamishi yao. Kampuni hizo ni pamoja na Sportspesa, Betin, Betpewa na Betways.

Waziri Msaidizi wa Fedha Nelson Gaichuhie na Kamishna wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) Bi Elizabeth Meyo walihudhuria mkutano huo.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya BCLB Liti Wambua hawakuhudhuria licha ya kupata mwaliko wa kamati hiyo.