Habari

Majambazi wavamia waombolezaji na kuiba pesa za mazishi

August 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

WAIKWA MAINA na BENSON AMADALA

FAMILIA moja inayoomboleza kifo cha mpendwa wao katika eneobunge la Kinangop, Kaunti ya Nyandarua, ilipata majonzi zaidi baada ya kuvamiwa na majambazi walioiba Sh18,000 zilizotengewa ununuzi wa jeneza la kuzika marehemu.

Bw Rufa Thiga, mkewe na nduguye walivamiwa na majambazi sita mnamo Jumatano usiku, saa chache tu baada ya waombolezaji waliofika kwao kuwafariji kutokana na kifo cha dada yao kuondoka.

Mkewe Bw Thiga, Margaret Wambui na nduguye Benson Kigo walijeruhiwa kwenye kisa hicho.

Bw Thiga alisimulia jinsi alivyowasikia majambazi hao waking’ang’ana kuvunja lango kuu la kuingia boma lake na jinsi jaribio lake la kutorokea mlango wa nyuma lilivyogonga mwamba.

“Nilipojaribu kutorokea mlango wa nyuma, watu wawili walinivamia kwa panga huku wengine wakiingia ndani ya nyumba na kumpiga mke wangu kwa silaha butu,” akasema Bw Thiga.

Baada ya hapo walimwagiza aingie ndani ya nyumba na awakabidhi pesa ambazo zilikuwa zimekusanywa kugharimia mazishi ya dadake.

“Walinilazimisha kuingia ndani ya nyumba niwape pesa za matanga. Niliwapa Sh18,000 ambazo zilikuwa zimetengewa ununuzi wa jeneza la marehemu,” akaongeza Bw Thiga.

Bi Wambui naye kwa masikitiko alisimulia jinsi majambazi hao walivyomfuata hadi kwenye bafu na kumpiga wakidai awape pesa. “Walitishia kuua familia yote. Nilipata majeraha kwenye mikono, mgongo na kichwani,” akasema.

Bw Kigo naye alisema kuwa wezi hao walimlazimisha aingie ndani ya nyumba na akawapa Sh3,000 ili kunusuru maisha yake. “Walinieleza kwamba walikuwa maafisa wa polisi kabla ya kunipiga kichwani na kuniamrisha nilale chini,” akasema Bw Kigo.

Kwingineko, wakazi wa kijiji cha Shiswa, eneobunge la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega bado wanaendelea kuomboleza baada kijana kumuua babake mwenye umri wa miaka 80 kutokana na mzozo kuhusu mlo wa ugali na mahindi choma.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 alitoroka baada ya kumuua babake.

Kulingana na wanakijiji, mshukiwa huyo mapema mwaka huu alichimba kaburi kwenye boma baada ya kuzozana na babake na kutishia kumuua na kumzika hapo.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Shinyalu, Robert Makau alisema polisi wanaendelea kumsaka mshukiwa huku uchunguzi ukiendelea kuhusu kisa hicho.