Habari MsetoSiasa

Sonko aitwa na EACC kuhusu matamshi

August 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

MATAMSHI ya Gavana wa Nairobi, Mike Sonko kumhusu Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo Bi Esther Passaris yamerudi kumwandama.

Bw Sonko alikuwa amedai kuwa Bi Passaris alidai marupurupu kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi baada ya kuzuru Amerika kinyume cha sheria

Alhamisi, Bw Sonko alifika katika ofisi za Tume ya Maadili na Kupambana na ufisadi (EACC) na kuhojiwa na wapelelezi Pius Ndiwa na Abdurizak Abduba kuhusu madai hayo.

EACC ilimuita gavana huyo kufafanua matamshi aliyotoa siku ya Madaraka Dei mwaka huu.

Tume hiyo ilisema kwamba inachunguza mienendo ya Bw Sonko kama mtumishi wa umma kufuatia madai aliyotoa dhidi ya Bi Passaris.

Bw Sonko alisema alikataa kulipa marupurupu hayo kwa sababu ziara ya Bi Passaris ilikuwa imefadhiliwa na bunge.

EACC ilisema ilimuita Bw Sonko kuandikisha taarifa kuhusu madai hayo na pia kumhoji kuhusu madai ya ufisadi.

Baada ya Bw Sonko kutoa matamshi hayo, Bi Passaris aliomba EACC kufanya uchunguzi akiapa kuwa hatakubali maadili yake kupakwa matope kwa misingi ya madai ya uongo.

Bi Passaris alitaja madai ya Bw Sonko kama uongo mtupu na akajipeleka katika ofisi za Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), EACC na Tume ya Uwiano wa Kitaifa (NCIC) kulalamika na kutaka yachunguzwe.

Jana, Bw Sonko aliyefahamishwa kuitwa kwake akihudhuria ibada ya wafu ya aliyekuwa Gavana wa Bomet, Dkt Joyce Laboso na aliyekuwa mbunge wa Kibra Ken Okoth, alisema atatii agizo hilo.

Na punde tu baada ya kuhutubia waombolezaji katika ibada ya kumkumbuka Bw Okoth katika shule ya wasichana ya Moi, mtaani Kibra, Bw Sonko alielekea katika ofisi za EACC katika jumba la Integrity Center.

Kwenye taarifa aliyotoa baada ya kupokea agizo hilo, Bw Sonko alisema iwapo EACC itapata alihusika na ufisadi, atajiuzulu.

Hata hivyo, alionya wale wanaoweza kufurahishwa na hatua hiyo kwamba hatakubali wizi wa pesa za umma.

“Ninajua kwamba kuna wanaofurahia hatua hii wakifikiri watarudi kupora mali ya umma lakini poleni sana. Nitakuwa nikifuatilia kwa karibu miradi yote niliyoanzishwa nikiwa nje ya ofisi,” alisema.