• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
Laboso, Okoth wamiminiwa sifa ibada ya wafu

Laboso, Okoth wamiminiwa sifa ibada ya wafu

NA LEONARD ONYANGO

WAKENYA wakiwemo viongozi wa kisiasa, Alhamisi waliungana kutoa risala zao kwa familia za aliyekuwa Gavana wa Bomet Joyce Laboso na mbunge wa Kibra Kenneth Okoth walioaga dunia wiki iliyopita kutokana na maradhi ya saratani.

Viongozi waliozungumza wakati wa maombi ya wafu yaliyofanyika katika Kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi, walimtaja Dkt Laboso kama kiongozi mkakamavu na mwenye busara aliyekuwa na kipaji cha uongozi. Naibu wa Rais William Ruto alimtaja Laboso kama mwanamke mkakamavu na mchapakazi aliyejitolea kutumikia waliomchagua.

Naibu wa Rais pia alifichua kuwa hospitali alikolazwa Dkt Laboso jijini London, Uingereza, walikuwa wamemwambia kuwa alisalia na siku chache za kuishi.

“Baada ya madaktari wa London kusema hivyo, nakumbuka tulijadili suala hilo usiku wa manane na tukaamua Laboso arejeshwe nyumbani,” akasema Dkt Ruto.

“Tulifanya mkutano wa dharura na Bi Anne Waiguru (Gavana Kirinyaga), Rachel Shebesh pamoja na familia yake ambapo tulijadili namna ya kuokoa maisha yake. Hapo ndipo tuliamua tumpeleke India. Familia na marafiki tulijaribu kadri ya uwezo wetu kuokoa maisha ya Joyce lakini haikuwezekana,” akaongezea.

Mkewe Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Bi Ida Odinga alisema Dkt Laboso alikuwa mwanafunzi wake katika shule ya upili.

Bi Odinga alisema urafiki wake na Dkt Laboso ulinoga pale alikutana na baba yake katika eneo la Sotik gari lake lilipoharibikia njiani akielekea Migori.

“Gari langu liliharibikia njiani na ghafla mwanaume akasimamisha gari lake akaambia dereva wake anitengenezee. Baadaye alinisihi niende kulala kwake na hapo ndipo urafiki baina yangu na familia ya Laboso ulianza,” akasema Bi Odinga.

Bw Bryan Abonyo, mmoja wa wana wa Dkt Laboso alimwita mama yake: “Malaika hapa duniani aliyetufanyia kila kitu kwa kujitolea.”

Gavana wa Kitui Charity Ngilu alisema kifo cha Laboso lilikuwa pigo kwa viongozi wanawake.

Katika ibada ya wafu iliyofanyika katika Shule ya Wasichana ya Moi jijini Nairobi viongozi walimtaja Bw Okoth kama mchapakazi, mwadilifu, mpenda watu na kiongozi mwenye busara.

Mjane wake Bi Monica Okoth alisema Ken alikuwa mkakamavu, mwenye busara, mcheshi.

“Nilikutana naye miaka 21 iliyopita tulipokuwa chuo kikuu.

“Nashukuru watu wa Kibra kwa kumchagua mara mbili kuwa mbunge wenu. Watu wa Kibra wamekuwa wakinikaribisha katika nyumba zao na nitaendelea kuwatembelea kwa sababu hapa ndipo nyumbani kwangu,” akasema.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen alisema Okoth alikuwa rafiki ya kila mtu bila kujali mipaka ya chama au kabila.

“Kuna wakati chama cha ODM kilidhani alikuwa amehamia Jubilee kwa sababu alikuwa anapenda kila mtu bila kubagua,” akasema Bw Murkomen.

“Ken alikuwa mtafiti mkubwa na ndiyo maana alitushawishi kuhalalisha bangi kwa ajili ya matibabu,” akaongezea.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko: “Ken alikuwa rafiki yangu mkubwa sana. Alikuwa mtu mchangamfu na alikuwa mtu anayejali urafiki.

“Magavana Laboso na Bw Okoth walikuwa na bima ya matibabu. Hata kama wangemaliza bima zao tungewachangia. Lakini tukumbuke kuna wananchi wa mapato ya chini wasioweza kupata chakula,” akasema.

You can share this post!

Sonko aitwa na EACC kuhusu matamshi

Wakulima waondolewa hofu ya uhaba wa mbegu za mahindi

adminleo