Wataalamu wapuuza dai la ‘mursik’ kusababisha saratani
Na EDITH CHEPNGENO
WATAALAM kuhusu ugonjwa wa saratani wamepuuzilia mbali hofu inayohusisha mursik ambayo ni maziwa yaliyogandishwa, na saratani ya koo.
Wataalam hao wamefafanua kwamba hakuna utafiti thabiti uliofanywa unaotangaza mursik kama chanzo cha maradhi hayo.
“Katika utafiti wowote, mbinu ambayo imetumiwa na mtafiti ili kufikia hitimisho lake ndiyo muhimu zaidi. Kulipatikana kemikali yoyote katika mursik?” aliuliza Dkt Elias Melly, daktari wa ugonjwa wa saratani katika Alexandria Cancer Centre
Kulingana na data ya utafiti wa Idara ya Kitaifa ya Usajili wa Saratani katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kimatibabu (Kemri) uliofanywa katika kaunti nne ikiwemo Nairobi, Mombasa, Bomet na Meru, asilimia 30 ya wanaume eneo la Bomet wanaugua saratani ya mfereji wa kupitishia chakula, asilimia 18 wanaugua saratani ya korondani huku asilimia 12 wakiugua saratani ya tumbo.
Miongoni mwa wanawake, saratani ya mfereji wa kupitishia chakula inaongoza kwa asilimia 22 ikifuatiwa na saratani ya uke kwa asilimia 5.6. Saratani ya matiti, utumbo mkubwa, utumbo mdogo na tundu la kupitishia haja kubwa inashikilia nafasi ya tatu kwa pamoja kwa asilimia 3.9.
Unywaji mara kwa mara wa mursik, umetajwa kama kiini kikuu cha saratani ya mfereji wa chakula katika maeneo ya Bonde la Ufa na Kaskazini mwa Kenya.
“Kabla ya kusema mursik ni chanzo cha saratani tunahitaji kufanya utafiti utakaochukua zaidi ya miaka mitano,” alisema Bw Naftali Busakhala, daktari wa maradhi ya saratani Eldoret.