Wakazi Gatundu Kaskazini wahakikishiwa fidia yao ya bwawa la Kariminu

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Gatundu Kaskazini wamepewa hakikisho la kupokea fedha zao zote za fidia kabla ya uzinduzi wa bwawa la Kariminu unaotarajiwa wakati wowote.

Waziri wa Maji Bw Simon Chelugui alisema hakuna mkazi yeyote atakosa kulipwa haki yake kabla ya mradi huo kuzinduliwa.

“Tunaelewa vyema kuwa wakazi wengi tayari wamepokea haki yao ya malipo katika awamu ya mwanzo. Wale wachache ambao bado hawajapokea fedha ni wale waliokuwa na matatizo ya maswala ya mashamba ya kifamilia na kwa hivyo sharti wasuluhishe mizozo kama hiyo,” alisema Bw Chelugui.

Alisema familia 246 zilipokea takribani Sh576 milioni kama fidia ya malipo ya kuhamia kwingineko.

Alisema kampuni ya maji ya Athi Water Service Board itafanya juhudi kuona ya kwamba wakazi wanaoishi katika maeneo ya juu ya milima wanavutiwa na kusambaziwa maji bila kuchelewa.

Alisema mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi wa maeneo ya Thika, Ruiru, Gatundu, na hata Kiambu ambapo wakazi wapatao 850,000 watanufaika pakubwa na usambazaji wa maji hayo mara tu ukishakuwa tayari.

Alieleza ya kwamba eneo litakalozinduliwa mradi huo ni la ekari 171 ambapo kampuni moja ya China ndiyo imepewa kandarasi ya mradi huo.

Alisema kulingana na mpangilio uliopo Tume ya Ardhi Nchini (NLC) ndiyo imepewa jukumu la kulipa fidia wakazi hao.

Kuanza kazi

Alisema maafisa wapya katika afisi hiyo wanastahili kuanza kazi yao rasmi kwa muda wa mwezi mmoja ujao, kwa sababu maafisa wa hapo awali muda wao umekamilika.

“Iwapo nyinyi wakazi wa hapa Gatundu mnayo shida yoyote, mna ruhusa kuja katika afisi yangu jijini Nairobi ama ile ya ardhi ili maswala yenu yaweze kutatuliwa,” alisema Bw Chelugui.

Alisema ni vizuri mradi huo kuendelea kwa sababu watu wengi watapata kazi kwa wingi.

“Kuna wale watauza chakula, wengine watapata tenda ya mchanga, kokoto, vyuma, na hata saruji. Kwa hivyo, kila mmoja wenu atapata kujiendeleza kimaisha,” alisema Bw Chelugui.

Mkazi mmoja wa eneo hilo, Bw George Muthua alisema wengi wao bado wanahitaji malipo yao ya fidia kwa sababu kwa sababu wanahitaji haki yao.

“Kuna wengine wetu hapa hawajapata haki yao na kwa hivyo, vile uko hapa waziri tunataka hakikisho kuwa tutapata fedha hizo haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Muthua.

Mkutano huo wa Alhamisi ulihudhuriwa pia na wahandisi wa mradi huo wa Kariminu, mbunge wa eneo hilo Bi Wanjiku Kibe na maafisa wakuu wa serikali.

Habari zinazohusiana na hii