Kimataifa

Rais, mpinzani wake watia saini mkataba kuzima vita Msumbiji

August 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA na MWANGI MUIRURI

MAPUTO, MSUMBIJI

RAIS wa Msumbiji Filipe Nyusi na kiongozi wa chama cha upinzani cha Renamo, Ossufo Momade Alhamisi walitia sahihi mkataba wa kihistoria kumaliza vita vilivyodumu kwa miongo kadhaa, runinga ya serikali ilitangaza.

Hafla hiyo ilifanyika katika mbuga la Gorongosa katikati ya Msumbiji, miaka 27 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kumalizika nchini humo.

Viongozi hao wawili walikumbatiana kwenye jukwaa baada ya kutia sahihi mkataba huo.

Kulingana na picha za runinga, nyuma ya jukwaa kulikuwa na maandishi yaliyosema “Amani: mkataba wa mwisho wa kumaliza uhasama.”

Mkataba wa Ijumaa ulitia kikomo juhudi za kuleta amani katika nchi hiyo zilizochukua muda mrefu ambazo zilianzishwa na aliyekuwa kiongozi wa Renamo, Afonso Dhlakama.

Dhlakama alifariki Mei 2018.

Uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba katika nchi hiyo.

“Tunataka kufahamisha watu wetu na ulimwengu kwamba tumezika mawazo ya kutumia vita kama njia ya kutatua tofauti zetu,” alisema Momade, alirithi uongozi wa Renamo kutoka kwa Dhlakama.

Nyusi alisema: “Mkataba huu unafungua enzi mpya katika historia ya nchi yetu kwamba hakuna raia wa Msumbiji anayefaa kutumia silaha kutatua mizozo. Kitendo ambacho tumeshuhudia kinaonyesha kujitolea kuwa na amani ya kudumu. Leo, Agosti 1, mimi ni mtoto aliyezaliwa upya.”

Punde tu baada ya Msumbiji ilipopata uhuru kutoka Ureno 1975, Renamo ilipigana na serikali ya chama cha Frelimo kwa miaka 16.

Watu milioni moja waliuawa kabla ya vita kumalizika 1992.

Waasi hao walijiunga na siasa baada ya 1992 baada ya mkataba wa amani uliotiwa jijini Roma na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ukafanyika 1994.

Renamo kilishindwa kwenye uchaguzi huo na zilizofuata na kikawa chama rasmi cha upinzani.

Mnamo Oktoba 2013 Renamo kilitangaza mwisho wa mkataba wa amani wa 1992 baada ya jeshi kuvamia kambi yake katika msitu wa Sathundjira.

Vita vilizuka upya kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa Renamo kuanzia 2013 hadi 2016.

Tangu 2016, serikali na Renamo zimekuwa zikiandaa mazungumzo ambayo yaliendelea baada ya kifo cha Dhlakama.

Licha ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kundi hilo kugeuka kuwa chama cha kisiasa, kilidumisha wapiganaji wake.

Njogu Wa Nganju ni Mhadhiri wa Somo la Sayansi ya Siasa katika Chuo kikuu cha Nairobi Picha/ Mwangi Muiruri

Ni hali sawa na ile ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM nchini Kenya, Raila Odinga kusalimiana Machi 2018 na kuamua kufanya kazi pamoja,

Mhadhiri wa Somo la Sayansi ya Siasa, Njogu Wa Nganju amesema kuwa “ona sasa ujinga wa Wakenya wengine kupinga handisheki hapa Kenya huku ikitumika kuleta amani kwingine.”

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro ameshabikia hali hiyo akiitaja kama ya kufana na ambayo inaunda mianya zaidi ya Wakenya kujipenyeza lakini kinaya ni kwamba, hapa Kenya, yeye ni mpinzani mkuu wa hendisheki kati ya Uhuru na Odinga.

Mwingine ambaye Taifa Leo imeuliza atoe maoni kuhusu hali hii ya Msumbiji ni mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri ambaye amesema amani ni ya maana.

“Amani ambayo inapaliliwa kwa njia isiyo na shaka,” amesema Ngunjiri.

Amesema ikiwa amani hiyo ya Msumbiji itaafikiwa kwa msingi wa haki na ukweli, bila wengine kucheza kamari ya kisiasa na suala hilo, basi ni sawa, lakini ikiwa ni hali kama ya “hapa kwetu ambapo maridhiano ni utapeli na hadaa, basi ninapinga.”