NHIF kulipa bili za wanafunzi wanaojifungua
NA FAITH NYAMAI
WATAHINIWA wa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE ambao watajifungua wakati wa zoezi hilo, watapokea huduma za kimatibabu kupita Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF).
Kulingana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, maafisa wa elimu nyanjani watashirikiana na maafisa wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) na vituo vya kimatibabu maeneo yao, ili kuhakikisha watahiniwa wajawazito wananufaika na bima maalum iliyoanzishwa na serikali kwa wanafunzi wote wa shule za umma mwaka uliopita.
“Nimewaagiza maafisa wote wa elimu nyanjani washirikiane na vituo vya kimatibabu na NHIF ili watahiniwa wajawazito ambao watahitaji huduma zozote wakati wa mtihani wasaidiwe kupitia kliniki za muda chini ya mpango wa bima ya NHIF Edu Afya kwa shule za umma,” akasema Prof Magoha.
Waziri huyo alikuwa akizungumza katika shule ya msingi ya Nairobi wakati wa mazungumzo kuhusu mtaala mpya.
Amri ya Prof Magoha inatarajiwa kumaliza utata kuhusu suala la wanafunzi wanaopachikwa mimba shuleni uliozuka mwaka jana kati ya serikali na NHIF.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NHIF wakati huo, Geoffrey Mwangi mwaka uliopita alisema wanafunzi wanaopachikwa mimba shuleni hawangenufaika na bima hiyo na kuwashauri kujisajili kwa bima ya Linda Mama au wajilipie gharama zote za kimatibabu.
Hatua hiyo ya Serikali inatarajiwa kuwasaidia wanafunzi wengi ambao huathirika kwa kukosa matibabu mwafaka.
Idadi ya wanafunzi wanaopata mimba za mapema imekuwa ikiongezeka nchini, na mwaka jana waliojifungua wakati wa mitihani walikuwa wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi.