Ripoti ya BBI kutayarishwa kuanzia leo, Haji atangaza
Na STEPHEN ODUOR
JOPOKAZI lililoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuzunguka nchini likikusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ya uongozi, Building Bridges Initiative (BBI), limekamilisha ziara zake katika kaunti 47.
Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa jopokazi hilo, Bw Yusuf Haji alisema wanakamati wamepanga kuanza kukutana faraghani Jumatatu ili kujumuisha maoni waliyopokea walipokutana na Wakenya mashinani.
Kulingana naye, kazi iliyobaki itakuwa ni kuchagua masuala yaliyotajwa sana na Wakenya kwa jumla ili kuchapisha ripoti mwafaka ya mapendekezo hayo.
Bw Haji alisema kuwa tayari walikuwa wamefanikiwa kupata maoni katika kaunti zote 47, yatakayozingatiwa kuamua kama kutahitajika kuwepo marekebisho ya katiba.
“Tumefanya lililopaswa na letu sasa ni kuchapisha nakala hiyo ya mapendekezo, ambayo itakuwa sauti ya Wakenya kwa jumla. Tutaiwasilisha kwa rais kabla wiki ya kwanza ya mwezi wa Septemba,” alieleza.
Timu hiyo inayojumuisha pia msomi wa masuala ya kisiasa, Adams Oloo, Seneta wa Busia Amos Wako, Said Mwaguni, Ole Ronkei na mhubiri Agnes Muthama , ilishiriki mjadala wa mwisho na wakazi wa Tana River, mjini Hola ambapo wakazi pamoja na viongozi walichangia maswala muhimu walioridhia yasajiliwe kama matakwa.
Mjadala huo ulishuhudia viongozi wa kaunti ya Tana River wakipendekeza mfumo wa uongozi utakaojumlisha viongozi kutoka kata zote za nchi katika ngazi za juu,wakiongozwa na rais atakayechaguliwa na wananchi.
Kamati ya BBI imepiga hatua hiyo kubwa wakati ambapo mapendekezo ya Chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa na Dkt Ekuru Aukot kurekebisha katiba, yanazidi kupata pingamizi.
Kufikia sasa, vyama vikubwa vya upinzani ikiwemo ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, na Wiper kilicho chini ya Bw Kalonzo Musyoka vimesema havitaunga mkono mapendekezo ya Dkt Aukot katika mswada wa ‘Punguza Mizigo’.
Vilevile, kuna malalamishi yaliyowasilishwa mahakamani kuzuia mswada huo wa Punguza Mizigo kujadiliwa na madiwani, ambao wengi wao wametangaza wataupitisha.
Miongoni mwa sababu zinazotolewa na wapinzani wa Punguza Mizigo ni kwamba, mswada huo haujatoa nafasi ya kubadilisha mfumo wa uongozi kitaifa.