• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Madaktari wa Cuba waliotekwa bado hawajulikani waliko

Madaktari wa Cuba waliotekwa bado hawajulikani waliko

Na MANASE OTSIALO

HATIMA ya madaktari wawili wa Cuba waliotekwa nyara Aprili 12 mwaka huu na watu walioshukiwa kuwa magaidi wa Al Shabab, haijafahamika.

Walipotekwa, Serikali ilisema Landy Rodriguez na Herera Correa walivukishwa hadi nchi jirani ya Somalia na kuwa wazee wa kijamii walikuwa wakitumiwa kusaidia kuachiliwa huru kwa madaktari hao.

Lakini baada kwenda eneo la El-Adde nchini Somalia, ambako iliaminika madaktari hao walikuwa wamezuiliwa, wazee hao walirudi Kenya mikono mitupu.

“Tulikwenda El-Adde kwa sababu hapo ndipo tuliambiwa madaktari wetu walikuwa wamefichwa,” Mzee mmoja aliyesafiri na kundi hili alidokezea Taifa Leo.

Mzee huyo alisema kundi la Al-Shabab walilokutana nalo El-Adde lilikanusha kuteka nyara madaktari hao lakini lilikiri kuwa nao katika ngome yao.

“Wale wa El-Adde walikanusha kuteka nyara madaktari hao mjini Mandera, na walidai waliletekwa na kundi lingine kutoka Mandera,” alisimulia Mzee huyo.

Hatua iliyofuata ni kuondolewa kwa madaktari wa Cuba waliokuwa wakihudumu katika kaunti za Wajir, Garissa, Tana river na Lamu kwa hofu pia hata wao wangetekwa. Mwezi uliopita, Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Macharia Kamau alisema juhudi zingali zinaendelea kuhakikisha madaktari hao wameachiliwa wakiwa salama.

Kundi la wazee lililotumwa Somalia lilisema madaktari hao walikuwa salama na walikuwa wakitoa matibabu nchini Somalia.

“Tuliwaona madaktari hao katika kambi moja ya Al-Shabaab. Tulikubaliana kuwa majeshi ya Kenya hawatashambulia ngome zao hadi mambo fulani yafanyike,” alisema mzee huyo.

Habari za ujasusi zinaonyesha madaktari hao walitekwa nyara na wahalifu fulani mjini Mandera na kisha kupeanwa kwa kundi la Al Shabab. Duru za kijasusi zilisema madaktari hao walifikishwa katika msitu wa Halaanqo karibu na mji wa Barawe na kisha kuslimishwa kwa lazima.

Maafisa wa usalama katika Kaunti ya Mandera wanalaumu serikali ya kaunti kwa utekaji huo, wakisema walikataa kushirikiana na polisi kuhakikisha usalama wa madaktari hao.

You can share this post!

Ghadhabu Pwani agizo la SGR likianza

Wasia wa mfu utakuwa ukizingatiwa utata ukiibuka –...

adminleo