Habari Mseto

Noti za Sh1000: Gavana wa CBK awataka Wakenya kuchukua tahadhari kuu

August 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Patrick Njoroge ameonya Wakenya kuwa muda hautaongezwa wa makataa ya uhalali wa noti ya zamani ya Sh1,000 ambayo ni Septemba 30.

Ina maana kuwa ni lazima uwe huna noti hiyo kwa hifadhi yako taslimu kuanzia saa sita usiku wa Septemba 30.

Njoroge ametoa hakikisho kuwa noti mpya ziko kwa wingi.

Licha ya kuwa serikali huwa na mazoea ya kuongeza muda wa makataa ya aina hiyo, gavana huyo Jumanne amewataka Wakenya wachukue tahadhari na wachunge kujipata na noti hizo mnamo Oktoba mosi kwa kuwa zitakuwa karatasi tu.

“Wewe chunga na uchukue tahadhari. Tumeziba mianya ya mafisadi ambao wanahifadhi noti hizo kwa magunia nyumbani mwao. Tunajua wanajaribu juu chini kuzibadilisha na hapo ndio hatari iko ya raia kujipata na noti hizo baada ya makataa hayo,” amesema Njoroge.

Akiwa katika harakati za uhamasisho ndani ya kituo cha redio cha Kameme, amesema kuwa mbinu ambazo mafisadi hao wanatumia ni kukopesha pesa zao kwa umma, kununua mali pesa taslimu na pia kuzipeana kwa madalali wakabadilishiwe kwa ama benki au kwa mitambo ya huduma za pesa kupitia simu za rununu.

“Hiyo ni sawa na kutekeleza uhalifu wa kusafisha pesa. Wanakusukumia shida zao kwa kuwa utajipata ndani ya mikopo, ukiandamwa na polisi au ukilemewa kubadilisha pesa hizo na hivyo upate hasara,” amesema.

Ameonya pia wakora ambao wanaunda pesa bandia kuwa serikali inawasaka kwa hali na mali “kwa kuwa hao ni sawa na magaidi wa kiuchumi.”

Amefafanua kuwa noti zile zitapigwa marufuku kuanzia Oktoba Mosi ni zile tu za Sh1,000.

“Ningetaka Wakenya waelewe kuwa noti zingine zote za Sh50, Sh100, Sh200 na Sh500 sambamba na sarafu za vyuma zitaendelea kutumika. Marufuku kwa sasa yanahusu noti ya zamani ya Sh1,000,” akasema.