Polisi Mungiki wanavyotesa wananchi
Na MWANDISHI WETU
HUKU makundi ya wahalifu yakiendelea kuhangaisha raia, baadhi ya maafisa wa polisi wamebuni magenge yao ya kuchukua ada haramu.
Polisi hao wahuni wanawahangaisha wananchi hasa wafanyibiashara, wakidai pesa jinsi kundi hatari la Mungiki lilivyokuwa likifanya.
Biashara wanazolenga ni matatu, vibanda, mabaa na bodaboda.
Wanaokosa kutoa ada hizo huadhibiwa jinsi Mungiki walivyokuwa wakifanya, lakini maafisa hao hutumia mamlaka yao kwa kuwasingizia makosa wananchi, kuwapiga na kuwafungia seli kisha wanaachiliwa wakitoa hongo.
Polisi hawa huzusha hofu miongoni mwa raia kila wanapoonekana na hubidi wawape pesa ili wasichukuliwe hatua hata kama hawana makosa.
Katika mtaa wa Donholm jijini Nairobi, wafanyabiashara waliambia Taifa Leo kuwa kila siku maafisa wanaotembea kwa makundi huanza kupiga doria mwendo wa saa moja usiku.
Doria hiyo si kwa minajili ya kuwapa wananchi usalama, bali ni kwa nia ya kukusanya ada ambazo mitaani zinafahamika kama ‘Protection Fees’ (ada za ulinzi).
Mwendo wa saa moja unusu usiku, polisi huonekana wakitembea kwa makundi ya wawili wawili, wake kwa waume, wakiingia katika biashara walizolenga kutoza ada hasa mabaa. Wote huwa wamevaa sare rasmi za polisi na kubeba bunduki.
Wamiliki wa baa, vilabu na maduka ya kuuza pombe waliozungumza na Taifa Leo walisema huwa wanalipa kati ya Sh200 na Sh500 kila usiku kwa maafisa hao.
“Ni hasara kwetu lakini hatuna namna nyingine. Ukikataa kulipa utatafutiwa kosa lolote lile na biashara yako itafungwa,” akasema mfanyabiashara aliyeomba kubanwa jina.
Katika mtaa wa Githurai 44, polisi hutumia gari rasmi na huwa wanaenda kutoka baa moja hadi nyingine. Wanapofika kwenye baa, mmoja ama wawili wanachungulia mlangoni, ambapo mhudumu hutoka nje na kuwapa “ada yao”.
Pia unapofungua biashara ya baa hubidi kuwahonga wakuu wa kituo kilicho karibu.
“Nilipofungua baa mtaani Githurai 45 ilibidi nitoe Sh20,000 kwa wakuu wa polisi eneo hilo. Kila anayefungua biashara hasa ya baa lazima atoe ada hiyo la sivyo utahangaishwa kila mara hadi utoe ama ufunge biashara,” akasema manyibashara mmoja.
Wahudumu walieleza kuwa unapotoa ada hizo haramu huwa unahakikishiwa usalama hata kama utaendelea kuuza baada ya saa zilizokubalika.
Imebainika utapeli huu hufanyika katika karibu kila mtaa jijini, hasa yenye makao ya wananchi wenye mapato ya chini na kadri na sio Nairobi tu bali pia katika miji mingine kitaifa na mashambani.
Kundi la Mungiki lilivuna mamilioni kutoka kwa wahudumu wa matatu wakati wa enzi zake. Lakini sasa polisi wa trafiki wamejaza pengo lililoachwa na sasa ndio wanahangaisha wahudumu hao kwa kuchukua ada hizo.
Wahudumu wa matatu Nairobi, Murang’a, Kiambu, Mombasa na maeneo mengine walieleza kuwa imekuwa kawaida polisi wa trafiki kuchukua ‘protection fee” kila siku kutoka kwao.
“Wengine huwa na vijitabu vya kuandika waliolipa. Hapa Nairobi ada ya kawaida kwa kila gari ni Sh200. Usipolipa utatafutiwa makosa na kuharibiwa biashara,” akasema meneja mmoja wa shirika la matatu Nairobi.
Katika Kaunti ya Mombasa, maafisa kadhaa wa trafiki hulipwa na wasimamizi wa mashirika ya matatu kila wiki ili kuepusha matatu zao kuwekwa kizuizini.
Kwa kawaida matatu huwa zina wasimamizi wao wanaofahamika kama ‘meneja’. Ni jukumu la msimamizi kuhakikisha kuna afisa wa polisi anayelinda magari yale anayosimamia.
“Gari linapokamatwa na polisi fulani kwa kukosa kufuata sheria za barabarani, kile ambacho dereva anahitajika kufanya ni kumfahamisha meneja. Meneja atampigia simu afisa ambaye hupokea ada kutoka kwake, kisha huyu afisa atampigia polisi aliyekamata gari na kumshawishi aliachilie,” akasema.
Kulingana naye, ‘mshahara’ wa polisi huwa kati ya Sh2,500 na Sh5,000 kila wiki ikitegemea maelewano kati yake na msimamizi wa magari ‘anayolinda’. Kiasi hiki ni kikubwa ikizingatiwa kuna uwezekano polisi mmoja hutegemewa na wasimamizi kadhaa wa matatu kulinda magari yao.
Wakati Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alipoapishwa mamlakani Aprili, aliahidi kupambana na uozo uliokithiri katika idara ya polisi.
Hata hivyo, kufikia sasa juhudi nyingi zimeelekezwa katika kupambana na ufisadi wa polisi wa trafiki, huku mahangaiko ya wafanyabiashara mikononi mwa polisi yakisahaulika.