• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 9:55 AM
Wanahabari Waislamu wafadhili makao ya watoto Kibra

Wanahabari Waislamu wafadhili makao ya watoto Kibra

Na CECIL ODONGO

KAMA njia ya kushiriki kwenye miradi ya kuinua jamii, Chama cha Wanahabari Waislamu Jumanne kilitoa msaada wa kifedha kwa makao ya watoto mayatima ya Arayan katika Msikiti wa Makina, mtaani Kibra.

Ufadhili huo wa Sh100,000 ulitolewa na kampuni ya Safaricom ambayo imekuwa ikishirikiana na chama hicho kuendeleza miradi mbalimbali ya kuhakikisha Waislamu wasiojiweza katika jamii wanapata msaada ili waendelee na maisha yao kama raia wengine.

Mwenyekiti wa Chama hicho Juma Namlola na Mwekahazina Asha Khamisi waliongoza hafla ya kutolewa kwa hundi ya thamani hiyo mbele ya wasimamizi wakuu wa makao ya Arayan ambayo huwapa watoto mafunzo ya dini ya Kiislamu na pia kozi za kiufundi.

“Mwaka huu safaricom kwa ushirikiano na kampuni ya Oglive walituuliza kama chama tutambue miradi ya kijamii ya kupata ufadhili huu na bahati hiyo iliangukia Arayan. Walitupa Sh100,000 ili tuwafae nazo. Japo ni kidogo, naomba mpokee ili kusaidia katika malezi ya watoto hawa,” akasema Bw Namlola.

Bi Khamisi naye alishukuru Arayan kwa kuwapa hifadhi na mafunzo ya kidini mayatima hao, akisema kwamba wanahabari Waislamu kupitia chama hicho wataendelea kujishughulisha na miradi ya kuinua maisha ya wasiojiweza.

Wasimamizi wa Arayan wakiongozwa na Bi Amina Suleiman nao walishukuru kwa msaada huo na kuomba chama na mashirika mengine kuwasadia kupata shamba la kujenga makao mapya makubwa ili kuwawezesha kukidhi idadi ya juu ya mayatima.

You can share this post!

Densi yachangamsha katika tamasha za muziki

20 wajeruhiwa Mandera katika ajali ya barabara usiku

adminleo