20 wajeruhiwa Mandera katika ajali ya barabara usiku
Na MANASE OTSIALO
WATU 20 walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Kaunti ya Mandera baada ya basi walilokuwa wameabiri kupata ajali katika barabara ya Mandera-Rhamu.
Wengi wa waathiriwa walivunjika miguu na baadhi yao wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.
Katibu wa Kaunti ya Mandera Abdinur Hussein alisema kuwa hospitali hiyo iliwashughulikia waathiriwa hao kwa haraka.
“Madaktari na wauguzi wetu walichukua hatua za haraka kushughulikia waathiriwa na baadhi yao wameanza kupata afueni,” akasema.
Waathiriwa wawili walikuwa na majeraha mabaya na walikatwa mikono.
Bw Hussein alilaumu dereva wa basi hio kwa kusababisha ajali iliyosababisha wanaume 11 na wanawake tisa kujeruhiwa.
“Tunataka polisi wachunguze madereva wote wanaoendesha magari ya usafiri wa umma katika barabara za eneo hili kwani wengi wao ni wanaendesha wakiwa walevi,” akasema.
Bi Jackline Wanjiru, manusura, alisema gari hilo lilipinduka bila kugonga kitu chochote.
“Tuliondoka Mandera saa mbili jioni na tukapata ajali saa mbili baadaye. Gari lilikuwa likienda kwa kasi kabla ya kupinduka,” akasema.
Inadaiwa kuwa basi hilo la Moyale Liner lilikuwa likishindana na mabasi mengine manne ambayo pia yalikuwa yakielekea Mandera.
Mwathiriwa mwingine, Bw Alex Nderitu alisema basi lilikuwa limebeba watu na mizigo kupita kiasi.
“Basi hilo lina uwezo wa kubeba watu 52 lakini tulikuwa wengi zaidi ya hapo kwani abiria wengine walikuwa wamesimama ndani ya basi,” akasema.
Bw Mohamed Bardad, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mandera alisema kuwa afisi yake haijafahamishwa lolote kuhusiana na ajali hiyo.
Mmoja wa wafanyakazi katika mabasi ya kampuni ya Moyale Liner alisema kuwa usimamizi wa kampuni hiyo ndio unafaa kulaumiwa kwa sababu uliruhusu gari kuhudumu licha ya kuwa ilikuwa imeharibika.
“Basi hilo liliwasili jana jioni na leo asubuhi likarejea barabarani bila kufanyiwa ukarabati,” akasema mhudumu huyo aliyeomba jina lake libanwe ili kuepuka kusutwa na mwajiri wake.
Kwa kawaida, mabasi hukaa mjini Mandera kwa angalau siku moja likifanyiwa ukarabati kabla ya kuondoka kurejea jijini Nairobi.
Basi hilo lilikuwa miongoni mwa mabasi matano yaliyoondoka Mandera kuelekea Nairobi ambapo wengi wa abiria walikuwa wanafunzi na walimu wanaoelekea kwenye likizo baada ya shule kufungwa wiki iliyopita.